Askofu wa kanisa la Tanzania Field Evangelism(TFE) maarufu kanisa la Emmanuel la mjini Shinyanga Edson Mwombeki
Watanzania wametakiwa kuwa makini na watu wanaoibuka kila
kukicha wakijitangaza kuwania nafasi ya urais ili waende ikulu kwani baadhi yao
hawana sifa ya kuwania nafasi hiyo na wengi wao hawafanya lolote la maana hata
kwenye majimbo yao wananchi wanaendelea kuwa na maisha magumu kila kukicha.
Hayo yamesemwa na Askofu wa kanisa la Tanzania Field
Evangelism(TFE) maarufu kanisa la Emmanuel la mjini Shinyanga Edson Mwombeki wakati wa kuhitimisha siku
tatu kavu za maombi pasipo kula wala kunywa yaliyofanywa na wachungaji 40
kutoka mkoa wa Shinyanga lengo likiwa ni kuombea taifa amani ikiwemo kumwomba
mungu aliepushe taifa na watu ambao mungu hajakusudia wagombee urais.
Askofu Mwombeki alisema hivi sasa kuna wimbi la kila mtu
kujitangaza kuwania urais ili waende ikulu lakini baadhi yao hawana sifa hiyo hata
majimbo yao yamewashinda ,wameshindwa kuwaletea maendeleo wapiga kura wao.
Alisema nafasi ya urais ni nyeti sana hivyo haiwezi
kuchezewa na kila mtu hivyo kuwataka watanzania kuwa makini na watu hao wasije
kuliingiza taifa kwenye matatizo ikiwemo kupoteza amani iliyopo sasa.
“Kati ya waliotangaza nia ya kuwania urais wapo wenye
sifa,lakini kuna wengine hata majimbo yao yamewashinda,wengine wanadiriki
kutumia pesa zao kusaka urais,wengine kukimbilia kwa waganga wa jadi wakiamini
nguvu za giza zitawapatia nafasi za uongozi,hii ni hatari sana,tusipokuwa
makini taifa litaangamia”,alieleza Mwombeki.
Askofu Mwombeki alisema watu wengi wakati wa uchaguzi wamekuwa
wakitumia pesa zao na nguvu za giza kusaka uongozi na kuongeza kuwa katika
uchaguzi wa mwaka huu watashindwa kwa nguvu ya mungu na nguvu ya
wananchi(umma).
“Tunahitaji rais mzalendo na nchi yake mwenye hofu ya mungu bila kujali anatoka chama gani cha
siasa,atakayesimamia maslahi ya nchi , kusimamia rasilimali za nchi badala ya
anayetumia nafasi ya uongozi wake kujinufaisha mwenyewe,tunawashangaa
wanaolilia ikulu,sijui wanafuata nini huko,maana hata Hayati Mwalimu Julius
Nyerere aliwahi kusema mtu anayelilia kwenda ikulu siyo mzuri,anapaswa
kuangaliwa kwa makini”,alieleza askofu Mwombeki.
Askofu huyo alikitaka Chama Cha Mapinduzi kuwa makini na
wagombea wake na kisipokuwa makini kuweka kiongozi mzuri vinginevyo taifa linaweza kupata rais
atakayelipeleka taifa pabaya.
Hata hivyo mbali na kusema wapo watu wenye sifa ya kuongoza
nchi ya Tanzania,askofu huyo hakutaja majina yao na kuahidi kutaja majina yao
mwezi Februari mwaka huu wakati wa mkutano wa maombi wa maaskofu na wachungaji
kutoka kanda ya ziwa Victoria.
Askofu Mwombeki aliwaomba viongozi wenzake wa dini kufanya
maombi ya dhati kuiombea nchi amani hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea
kufanya matukio makubwa mawili ya kupigia kura katiba pendekezwa na uchaguzi
mkuu.
“Yapo matukio makubwa mawili yatafanyika hapa nchini,suala
la katiba na uchaguzi lakini tayari kuna dalili mbaya zinajionesha,sasa hivi
kuna kundi la wahalifu “Panya Road” linayumbisha nchi,tunapaswa kuwa makini
sana kwani nidhamu ya nchi imeanza kupotea”,aliongeza Askofu Mwombeki.
Katika hatua nyingine aliwataka watanzania kujitokeza kwa
wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura kwani ndiyo sehemu pekee
watakayoitumia kupata viongozi wanaowataka katika uchaguzi mkuu ujao.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Na Kadama Malunde-Shinyanga