Ndugu
wa marehemu akifanya yake kaburini,kulia ni kiboksi kilichokuwa
kimebeba kuku aliyechinjwa kisha kuwekwa kwenye tumbo la marehemu na
kuzikwa naye. |
Habari tulizozipata hivi punde katika chumba cha habari cha Malunde1 blog zinasema kuwa kumetokea vurugu za aina yake katika makaburi ya Masekelo katika manispaa ya Shinyanga wakati wa mazishi ya mwanamke mmoja aitwaye Benadetha Steven(35) aliyekuwa anaishi katika mtaa wa Mapinduzi maarufu mtaa wa Juma Matv katika kata ya Ndala aliyefariki dunia juzi wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga.
Tukio hili limetokea mchana huu wakati wa mazishi ya mwanamke huyo anayedaiwa kufariki dunia kutokana na uvimbe wa tumboni uliokuwa unamsumbua hivyo ndugu wa marehemu kuamua kumfanyia mambo ya kimila.
Habari zinasema kuwa ndugu wa mwanamke huyo anayetokea Musoma (Mkurya) walikuwa wanataka ndugu yao apasuliwe tumbo wafanye mambo ya kimila makaburini ili kuondoa mkosi katika ukoo wa lakini uongozi wa eneo husika wakasema utaratibu huo ni vyema ungefanyika hospitalini badala ya hadharani watu wakishuhudia.
“Mgogoro ulianzia nyumbani hata kabla ya kwenda makaburini,ndugu
walionekana kuelewa wakatulia na wakati mazishi yanaendelea ndipo ndugu mmoja
wa marehemu akaingia kaburini,akiwa amevaa mipira ya mkononi,akiwa na wembe na
boksi dogo lililokuwa na kifaranga cha kuku na kuzuia waombolezaji wasitupie
udongo kaburini”,alieleza mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la
Sijali Jumanne aliiambia Malunde1 blog.
"Ndugu huyo wa marehemu aliingia kaburini baada ya mchungaji kumaliza ibada ya mazishi na kuruhusu mwili wa marehemu ufukiwe,ndipo akaanza kuuchana kwa wembe,akachinja kuku,kisha kumwagia damu marehemu na kumwingiza kuku huyo kwenye tumbo la marehemu,akafunika jeneza na ndugu wakaendelea na mazishi”,aliongeza Jumanne.
Shuhuda huyo alisema kitendo cha ndugu wa marehemu kung'ang'ania kufanya
mambo yao ya kimila tena hadharani,kiliwakera wananchi wakaamua kutoka
makaburini,na jeshi la polisi likafika eneo la tukio na kuwakamata ndugu wote
wa marehemu.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mapinduzi Ayubu Daniel alikiri kuwepo kwa
tukio hilo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha ameiambia Malunde1 blog kuwa jeshi la polisi linafanya uchunguzi zaidi juu
ya tukio hilo.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin