Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini Kanali mstaafu Tajiri Maulid akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati akitoa tamko la Chama baada ya UVCCM Kufunga ofisi za Chama hich |
Tamko la Chama |
Akitoa tamko la kamati hiyo jana kwa waandishi wa habari
mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga Kanali mstaafu Tajiri Maulid alisema CCM inalaani na
imepokea kwa masikitiko makubwa juu ya jaribio la baadhi ya vijana wa UVCCM
kufunga ofisi kwa lengo la kuwazuia viongozi kuingia ofisini kwa madai
mbalimbali.
Tamko la kamati hiyo linakuja siku moja baada ya baadhi
ya vijana wa UVCCM kufunga ofisi za CCM wilaya wakishinikiza katibu wa wilaya
Charles Sangula,katibu wa siasa na uenezi wa wilaya Charles Shigino na mchumi
wa wilaya ya hiyo Ahmed Mapalala waondolewe katika chama.
Vijana hao walidai hawawataki viongozi hao, kwani
wamekuwa wakikiuza chama na kuwapa nafasi wapinzani, huku wakiwatolea kauli
mbaya na kuwazarua umoja huo wa vijana(UVCCM), hali ambayo wanahofia kukosa
viti vingi vya uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akitoa tamko hilo Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya alisema
wanalaani uasi huo na kudai kuwa kamati yao haiamini kama kitendo kilichofanywa
na vijana hao ni makubaliano ya UVCCM wilaya ya Shinyanga Mjini bali ni tamko
la watu binafsi.
“Ofisi ni mali ya taasisi siyo mali ya mtu kwa hiyo
kufunga ofisi maana yake huduma zisizitolewe,wao wametoa tamko binafsi,vikao
vyetu vitaona nini kifanyike juu yao,hawawezi kutoa tuhuma na kutoa adhabu,hii
siyo sawa,adhabu zinatolewa kwenye vikao vya chama,siyo kwa kundi la watu na
kukutana na kuanza kuropoka”,alisema Maulid.
“Kutoa tuhuma ni sawa,lakini njia waliyotumia siyo
sahihi,madai yao yanahitaji uchunguzi ndiyo maana sisi kama chama tunakaa vikao
kwa ajili ya uchunguzi,kamati ya siasa ya halmashauri ya kuu ya chama
imeelekeza kwa mwanachama yeyote ambaye atakuwa na tuhuma kwa kiongozi yeyote
afuate taratibu za kutumia vikao si vinginevyo”,aliongeza Maulid.
Hata hivyo alisema tayari vijana hao 24 waliofunga ofisi
za Chama wameandika barua wakielezea madai yao na kwamba uongozi wa CCM wilaya
unaendelea na uchunguzi juu ya madai yao na watatoa taarifa mara tu
watakapokamilisha uchunguzi wao.
Katika hatua nyingine alisema kamati yao inaendelea
kufanya uchunguzi juu ya tukio la vijana hao kumshushia kichapo diwani wa Kata
ya Ndala katika manispaa ya Shinyanga George Sungura(CHADEMA) aliyekatisha
katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga Mjini.
“Mimi sikuwepo wakati tukio hilo linatokea,lakini mpaka
sasa hatujapokea malalamiko yoyote kutoka kwa diwani huyo,hata hivyo sisi kama
chama tunafanya uchunguzi ili kujua undani wa tukio hilo”,aliongeza Maulid.
Social Plugin