Polisi
aliyetimuliwa kazi, Godfrey Mushumbusi (42), amewakata mapanga na
kuwajeruhi mama na mwanae kisa anawadai chupa mbili tupu za bia.
Sekela Mwiniwasa (44) na mtoto wake Ricado Dancan (24), mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walikatwa mapanga na kupigwa virungu maeneo tofauti mwilini wakiwa kwenye baa ya Itawa inayomilikiwa na askari huyo Alhamisi wiki hii.
Mkasa huo uliotokea Tabata Kisukuru, ulithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi na kusema kwamba chanzo ni familia hiyo kushindwa kupeleka chupa hizo kwa wakati na kulipa deni la Shilingi 10,000.
Alisema mtuhumiwa alifikishwa kituoni na kuachiwa kwa
dhamana na upelelezi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani.
Akisimulia mkasa huo, Sekela alisema Jumanne ya wiki hii alimwagiza mdogo wake, Leah Mwaipaja bia mbili kwenye baa hiyo na siku iliyofuata Mwaipaja alivyopita kwenye baa hiyo, mmoja wa wahudumu wake Sophia akamuuliza mbona hajarudisha chupa.
“Alimjibu ziko kwenye mfuko lakini amezisahau na kuahidi kuzipeleka,” alisema na kuongeza kuwa Sophia alianza kumporomoshea matusi ya nguoni kitendo kilichomsababisha arudi nyumbani na kumueleza mke wa Msumbushi aliyekuwa nyuma ya baa hiyo.
Alieleza kuwa wakati anarudi nyumbani, mhudumu huyo alimfuata na kumweleza kwa nini alitoa taarifa hizo kwa bosi wake na kuanza kumshambulia.
“Walipigana mbele ya baa hiyo na mke wa mtuhumiwa alikuwapo na kuwachochea kwa maneno ili ugomvi uendelee, lakini aliona haitoshi akachukua fimbo kumtandika nayo,” alisema.
Baada ya kipigo Mwaipaja alirudi nyumbani na kuelezea kichompata hivyo Sekela akalazimika kwenda naye kumaliza tatizo hilo lakini alijibiwa vibaya na Sophia na kuondoka.
“Nikiwa kwenye eneo hilo, mume wangu alipita akitokea kazini nilimsimulia kilichotokea kabla sijarudisha chupa hizo.
Baada ya kuzikabidhi nilianza kutukanwa na wahudumu matusi ya nguoni ambayo yalishuhudiwa na watoto wangu akiwamo aliyejeruhiwa,” alisema na kuongeza:
“Ricado alimshika mmoja wa wahudumu na kumuuliza kwa nini ananitukana, ndipo polisi huyo akanishika na kunipiga rungu kichwani hadi nikazirai na kisha kumkata mtoto wangu mapanga mikononi,” alisema.
Alisema askari huyo baada ya kuona amewajeruhi, alimwagiza mlinzi aliyekuwapo eneo hilo atoe mshale atumalizie lakini naye alikataa , wakati akiwakata mapanga aliwatishia kuwa kila jeraha watalazimika kulilipia kwa riba.
“Ninachokumbuka niliona watu wamejaa eneo la tukio na baadaye nilizirai nilipoamka nilikuwa hospitali ya Amana, nimeshonwa nyuzi saba kichwani na mwili wote unauma,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo, mtuhumiwa alipiga simu polisi na kudai amevamiwa na panya road ambapo gari la polisi lilifika lakini kutokana na maelezo yake kupishana, polisi walifanya uchunguzi na kubaini kuwa aliwadanganya.
“Alikutwa na mkewe wakiwa wamelowa damu, polisi waliwauliza hao panya road wamekujeruhi wapi, akadai walifika na kuanza kukatana mapanga wenyewe kwa wenyewe, wakakimbia, lakini mama mmoja aliyekuwepo eneo la tukio aliwaeleza ukweli wa mambo ndipo Msumbushi akapelekwa kituo cha polisi Stakishari,” alisema.
Na Romana Mallya-NIPASHE JUMAPILI