Maaskofu na wachungaji wamesema huenda mchakakato wa kupata katiba mpya
nchini ukakwama kutokana na kile kilichoelezwa kuwa maaskofu na wachungaji
wachache sana wana nakala za katiba inayopendekezwa hali ambayo
inawafanya wengi wao washindwe kuifafanua kwa usahihi mbele ya waumini wao.
Hayo yamesemwa na askofu wa kanisa la Tanzania Field
Evangalism (TFE) la mjini Shinyanga Edson Mwombeki wakati wa ibada ya mkesha wa
mwaka mpya 2015 iliyoenda sambamba na kufunga kongamano la siku 5 la wachungaji
na maaskofu 200 kutoka mikoa mbalimbali nchini lenye lengo la kuombea taifa na
kudumisha umoja katikati ya watumishi wa mungu.
Askofu Mwombeki alisema wachungaji na maaskofu wengi
walioko katika wilaya na mikoa mbalimbali nchini hawana katiba inayopendekezwa
kwa ajiri ya kupigiwa kura na wananchi mpaka sasa hali ambayo inazua hofu kwani
wanashindwa kuifafanua kwa wananchi na badala yake wanasiasa ndiyo wamekuwa
wakifafanua mambo ya katiba na kila mmoja akizungumzia kivyake.
“Huwezi kupigia kura kitu usichokielewa,maaskofu na wachungaji
wameniambia wanataka katiba,waweze kuzungumza na watu wao kitu sahihi,kwani
hivi sasa kila mwanasiasa anazungumza vya kwake,sisi tufanyeje sasa,hatutaki
serikali ifike kipindi cha kupiga kura halafu watu wapige ndiyo au hapana
wakati hawajaelewa,je wakipiga hapana wakati ilikuwa nzuri tutafanyeje?”alihoji
Mwombeki.
Alisema lengo lao siyo kukataa katiba wala kupigizana
kelele na serikali bali ni kusaidia kupatikana kwa katiba bora kutokana na
serikali kutumia gharama kubwa,na kama gharama imetumika basi serikali ione
umuhimu wa kugawa katiba pendekezwa bure.
“Tunapenda kumpongeza rais Kikwete kwa jitihada zake
nzuri za kuonesha demokrasia iliyo imara katika taifa la Tanzania ikiwa na
lengo la kuifanya nchi iendelee kuwa na amani,jambo ambalo amelifanya kwa bidii
na nguvu zake zote na kufikia hatua ya kupata katiba pendekezwa ambayo sasa
imefika hatua ya pili”,alieleza Mwombeki.
“Tunaomba rais Jakaya Kikwete atuamini,kama
tusingeiombea wangepigana Dodoma,kinachotuuma sisi wachungaji tulilala makanisani
tukiomba tukatuma wajumbe huko Dodoma hadi kufikia rais anaiinua katiba na
kusema ni nzuri,sasa asije akatudharau,tunataka atuletee ili tujue mapema kama
ni ya kuweka pembeni au la!,wanasiasa wanasema ni mbovu,sisi
tufanyeje,tuwaambiaje watu wetu”,aliongeza Askofu Mwombeki.
Kwa upande wake Mchungaji Valentine Martine kutoka
Missionary Pentecoste Church Karagwe mkoani Kagera alisema hivi sasa wanashindwa
kuelewa nini cha kuelimisha kwa wananchi kutokana na kutoelewa kichomo kwenye
katiba hiyo hivyo wanahitaji wapewe katiba inayopendekezwa bure.
“Kila mwanasiasa anaongea lake,lakini jamii inatuamini
sisi watumishi wa mungu,tukiisoma tukaielewa tutaipeleka kwa watu,sisi siyo
wanasiasa, tutasema yaliyo kweli bila kuipindisha wala uongo,wasomi wanasema
mwanasiasa mara nyingi wanaongea uongo,ukijua kweli utakuwa huru”,alisema
mchungaji Martine.
Naye mchungaji
George Daniel kutoka kanisa la
Pentecoste Assemblies of God Tanzania(PAGT) Bariadi mkoani Simiyu alieleza kuwa
anapata wasiwasi kusema katiba pendekezwa inafaa au la kutokana na kutojua
katiba hiyo ina manufaa kwa jamii au la.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba +255 688 405 951
|