Kali ya Shinyanga!! WAJAWAZITO WAKIMBIA HOSPITALI ETI KISA HAWATAKI KUZALISHWA NA WAUGUZI WENYE UMRI MDOGO

Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe(pichani) amesema akina mama wajazito 64 wamepoteza maisha katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba 2014 kutokana na sababu mbalimbali ikwemo akina mama wajawazito kutojifungulia hospitali kwa madai kuwa wanaona aibu kuzalishwa na wauguzi wenye umri mdogo.


Akizungumza na malunde1 blog jana ofisini kwake Dkt Kapologwe alisema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 50 ya akina mama mkoani Shinyanga hukimbilia kwa wakunga wa jadi na wengine kujifungulia majumbani hivyo kuwa hatarini kupoteza maisha yao kwa kukosa huduma muhimu.

Alisema mwaka 2014 kulikuwa na vifo 64 vya akina mama wajawazito mkoani humo huku mila na desturi zikichangia kutokea kwa vifo hivyo.

“Uchunguzi tulioufanya unaonesha kuwa  mila na desturi pia zinachangia vifo vya akina mama wajawazito,tumezungumza na akina mama wanasema wauguzi wengi siku hizi wana umri mdogo,hivyo wanaona aibu kuzalishwa na watoto”,alisema Dkt Kapologwe.

“Akina mama hususani wenye umri mkubwa wanadai wanaona aibu kuzalishwa na wauguzi wenye umri mdogo sawa na watoto wao,naomba wabadilike kwa sababu suala la umri siyo tatizo kwa sababu wauguzi wetu wamesomea kazi hiyo na wana utaalamu wa kutosha,na wakifanya hivyo tutapunguza vifo vya akina mama wajawazito”,aliongeza Kapologwe.

Alitumia fursa hiyo kuwataka akina mama wajawazito na wananchi wa Shinyanga kwa ujumla kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati na kutumia zahanati,vituo vya afya na hospitali zote zilizopo mkoani humo kwani huduma zinapatikana kwa saa 24.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na malunde1 blog baadhi ya akina mama walisema sababu zingine zinazowafanya wasijifungulie hospitali na badala yake kukimbilia kwa wakunga wa jadi ni kauli mbaya zinazotolewa na baadhi ya manesi.

“Unasafiri umbali mrefu kwenda hospitali kujifungua,unafika pale nesi anakutolea kauli mbaya,Wasukuma hawapendi kutukanwa ,unafikiri kwa hali hiyo siku nyingine nitarudi tena?”,alihoji Elizabeth John.

Naye Lilian Mwese alisema baadhi ya akina mama hawapendi kondo la uzazi kutupwa hospitalini tofauti na mila zao zinazowataka wayachimbie ardhini hali ambayo inawafanya waogope kwenda kujifungulia hospitalini.

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post