Kamanda wa Polisi wa Mkoa Singida, Thobias Sedoyeka
MKURUGENZI Mtendaji wa Wilaya (DED)
ya Iramba,mkoani Singida Halima Mpita (47) amenusurika kifo baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa bomu la kutengenezwa kienyeji.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka alisema mjini hapa jana
kuwa tukio hilo lilitokea Januari 2, mwaka huu saa 1.15 asubuhi wakati
mkurugenzi huyo akiwa nyumbani kwake, akijiandaa kwenda kazini huku
bahasha yenye mlipuko ikiwa juu ya kitanda.
Akisimulia
mkasa huo, Kamanda Sedoyeka alisema Desemba 30 mwaka jana saa 4.00
asubuhi, mkurugenzi huyo alipokea bahasha kutoka kwa katibu muhtasi wake
na alipoifungua alikuta ujumbe usemao: “Poleni sana, hatuwezi kufanya
‘dili’ la milioni 90 halafu mkala peke yenu, sisi katudhulumu
tukawaacha”.
Alisema
kuwa baada ya kusoma ujumbe huo, Mpita aliamua kwenda na bahasha hiyo
nyumbani kwake, bila kujua iwapo kulikuwa na kitu kingine ndani yake.
“Ilipofika
siku ya tukio (jana), akiwa anajiandaa kwenda kazini huku ile bahasha
ikiwa juu ya kitanda chake tayari kuichukua, alishitukia ikilipuka kwa
kishindo,” alisema Kamanda Sedoyeka.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, mlipuko huo ulitoboa godoro kiasi cha nusu inchi kwenda ndani na upana wa inchi mbili.
Alisema
kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na mlipuko
huo, lakini jeshi la polisi likishirikiana na wataalamu wa milipuko
kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanashughulikia
suala hilo.
Social Plugin