Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha Mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya |
Watu wanane ambao ni wachimbaji wadogo wa dhahabu wanahofiwa kufa kwa kufukiwa na udongo katika machimbo ya Kalole kata ya Lunguya Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga na mwingine kupigwa risasi ya tumbo na askari polisi katika ugomvi wa kugombea jiwe la dhahabu.
Wakati matukio
hayo yakitokea baadhi ya wachimbaji wamedai hali hiyo inatokana na jeshi la polisi
kutokuwa na ushirikiano na jamii ya maeneo hayo na kumtaka mkuu wa jeshi hilo
nchini kufanya mabadiliko ya haraka wilayani humo ili kunusuru dhana ya polisi
jamii.
Tukio
la
kwanza la wachimbaji hao kufukiwa na kifusi linadaiwa kutokea desemba 15
mwaka jana majira ya jioni wakati wachimbaji hao walipokuwa ndani ya
moja ya mashimo
yaliyopo katika eneo hilo la mgodi unaomilikiwa na Maulid wakati wakigombea
kuchimba mchanga
wa dhahabu.
Baadhi ya
wachimbaji wakiwemo Abduh Juma,John Mwita ambao ni wakazi wa Tinde Shinyanga na Nzega mkoani Tabora walisema kuwa baada ya wenzao kufukiwa walisitisha
shughuli zote za mgodi huo na kuanza kuwafukua wenzao kwa saa saba na kufanikiwa
kuokoa wachimbaji wawili waliowaopoa wakiwa hai kabla ya wachimbaji
waliookolewa kutoroshwa na polisi wasitoboe siri kwa wanahabari na mpaka sasa
hawajulikani walipo.
’’Baadaye na
sisi tulikata tamaa na kuamua kuwaacha wenzetu wakiwa shimoni maana kila
tuliyekuwa tukimfuata alitupuuza kana kwamba hakuna tukio lililotokea eneo lile’’,alisema
Juma kwa masikitiko.
Hata hivyo
siku iliyofuata kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo ikiongozwa na
mwenyekiti wake Benson Mpesya ilifika eneo hilo na kuahidi kuleta vifaa vya
uokoaji lakini haikufanya hivyo.
Hata hivyo
mkuu wa wilaya alipotafutwa hakukiri wala kukanusha kuwepo kwa tukio hilo na
badala yake alidai kuwa yuko jijini Mbeya msibani na kuahidi kuzungumzia tukio
hilo baada ya msiba huo kumalizika.
Kufuatia
hali hiyo,uongozi wa mgodi huo kwa kushirikiana na polisi umeamua kujenga
kaburi juu ya eneo waliofukiwa wachimbaji hao ili
kuzuia wachimbaji wengine kufika eneo hilo.
Mwenyekiti
wa wachimbaji wadogo mkoa wa shinyanga(SHIREMA) Nicodemus Majabi amekiri
kutokea kwa tukio hilo ila akakanusha idadi hiyo akidai waliofukiwa ni watatu
na wawili waliokolewa huku mmoja aliyemtaja kwa jina moja la Mussa ikishindikana
kumuokoa kutokana na udongo wa eneo hilo kuwa tifutifu.
‘’Hili
tukio lipo lakini waliofukiwa ni watatu na kati ya hao wawili waliokolewa na
mmoja ndiyo bado yupo ardhini imeshindikana kumuokoa kutokana na udongo kuwa
tifutifu’’alisema Majabi
Katika tukio
la pili mchimbaji Kulwa Kashinje(32) ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi
wakati wakigombea jiwe linalodhaniwa kuwa na dhahabu.
Tukio hilo
ambalo limetokea ndani ya mgodi huo unaodaiwa kufukia wachimbaji hao,limetokea Novemba 15,2014 mwezi mmoja kabla ya wachimbaji hao kufukiwa majira ya saa 12 jioni.
Imeelezwa
baada ya polisi huyo aliyefahamika kwa jina la utani la Cheupe kumpiga risasi
mchimbaji huyo alihamishwa kutoka katika kituo cha polisi wilaya ya Kahama na haijajulikana alikohamishiwa.
Kamanda wa
polisi Mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alidai hana taarifa za matukio hayo na
kuahidi kufuatilia ili kujua ukweli halisi wa matukio hayo mawili.
Na Valence Robert-Kahama