MBUNGE WA SHINYANGA MJINI AWACHEFUA WANANCHI

Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Shinyanga wamelalamikia kitendo cha kutokufunguliwa kwa ofisi ya mbunge wao, Stephen Masele hali ambayo wamedai inachangia kwa kiasi kikubwa wakose sehemu ya kuelezea kero mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.
 
Mbali ya kutokufunguliwa kwa ofisi pia wakazi hao wamelalamikia kitendo cha simu ya mbunge huyo kutopatikana muda wote pale anapotafutwa kwa njia ya simu na kwamba namba yake aliyokuwa ameitoa kwa wapiga kura mara baada ya kuchaguliwa ya 0767 286 000 hivi sasa haipo hewani kwa kipindi kirefu.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita wakazi hao walisema Jimbo la Shinyanga hivi sasa linaonekana kama halina mwakilishi kutokana na wakazi wake kukosa mtu wa kumfikishia matatizo yao baada ya mbunge wao kuteuliwa kushika wadhifa wa Naibu waziri wa nishati na madini.
 
Walisema pamoja na nafasi aliyopewa mbunge wao kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya jimbo lao lakini hata hivyo ingekuwa ni vizuri akaweka utaratibu mzuri utakaowawezesha wao kuwa na mawasiliano naye ya mara kwa mara kwa kuweka mtu mahsusi wa kukaa ofisi katika nyakati zote za muda wa kazi wa kiofisi.
 
Mmoja wa wakazi hao, Madeleke Stephen mkazi wa eneo la Chibe alisema wapiga kura wa jimbo la Shinyanga wanasikitishwa na kitendo cha kutofunguliwa kwa ofisi ya mbunge wao hali ambayo inasababisha wakose mtu wa kumweleza matatizo yao kutokana na simu za mbunge huyo kutokuwa hewani muda wote.
 
“Ukweli kitendo cha kutofunguliwa kwa ofisi ya mbunge kwa muda wote ni sawa na sisi kukosa mwakilishi, maana hatuna sehemu ya kufikisha matatizo yetu, kibaya zaidi hata njia rahisi ya mawasiliano ya simu imeshindikana, maana ni rahisi zaidi kupata simu ya Rais Kikwete (Jakaya) kulikoni ya mbunge Masele,” alieleza Stephen.
 
Kwa upande wake mmoja wa makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mjini Shinyanga ambaye hata hivyo hakupenda kutajwa gazetini alisema kitendo kinachofanywa na mbunge wao kinaweza kusababisha madhara makubwa kwa chama chake wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015.
 
“Ni kweli kuna malalamiko ya muda mrefu kuhusiana na suala la huyu mbunge wetu, wananchi wengi wamekuwa wakihoji kitendo cha ofisi yake kutofunguliwa mara kwa mara, awali alikuwa na msaidizi ambaye pia alikuwa ni katibu wa Jumuiya ya wazazi wa CCM, lakini hivi sasa huyu ameacha kazi hiyo,”
 
“Baada ya kuacha tunasikia ameajiriwa katibu mwingine, lakini ajabu bado wananchi wanakwenda katika ofisi yake wanakuta imefungwa, sijui hizi shida za jimbo zitapokelewaje? Ni haki wapiga kura kulalamika, tuna miezi michache kuelekea uchaguzi mkuu, sasa huyu bwana ajisahihishe asije kukipa wakati mgumu chama chetu wakati wa kampeni,” alieleza kada huyo.
 
Hata hivyo kwa upande wake msaidizi wa sasa wa mbunge huyo, Mwajuma Rabia alikanusha madai hayo na kueleza kwamba mara nyingi ofisi hiyo ipo wazi katika muda wote wa saa za kazi na kuwaomba wananchi wasisite kupeleka matatizo yao.
 
Kuhusu kutokupatikana kwa simu, Masele alikiri ni kweli muda mwingi amekuwa akifunga simu zake kwa vile iwapo ataziacha hewani itakuwa vigumu kwake kutekeleza majukumu mengine aliyonayo ya unaibu waziri wa Nishati na Madini na badala yake atakuwa na kazi ya kupokea simu za wapiga kura muda wote.
 
“Ni kweli kabisa simu zangu muda mwingi nazifunga, sipendi kuziacha wazi, maana waandishi ninyi wenyewe mnaelewa kwamba nafasi niliyonayo hivi sasa ninashughulikia watu wengi zaidi, hivyo iwapo nitaziacha hewani nitakosa muda wa kushughulikia mambo mengine, muda wote itakuwa ni masuala ya jimbo tu,” alieleza Masele.
 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post