Mwaka wa uchaguzi umeingia. Usiku wa kuamkia leo, Watanzania
wameupokea mwaka mpya 2015 huku tafakari kubwa ikiwa ni matukio makubwa
yatakayotokea mwaka huu, ukiwamo Uchaguzi Mkuu na kura ya maoni ya
Katiba Inayopendekezwa.
Mbali na uchaguzi wa rais wa awamu ya tano,
wananchi wataamua ama kuipitisha au kuikataa Katiba Inayopendekezwa,
mambo ambayo wasomi, wanasiasa na wanaharakati wameonya kuwa yanatakiwa
kuendeshwa na kusimamiwa kwa weledi na umakini mkubwa.
Vilevile, kutokana na matukio hayo kugharimu fedha
nyingi, wataalamu wa uchumi wanatabiri kuwa mwaka huu utakuwa mgumu na
itakaowalazimu Watanzania kufunga mikanda zaidi.
Pia, macho na masikio ya wananchi yako kwa vyama
vya upinzani ambavyo vimeungana na kuzaa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kuona kama vitasimamisha mgombea mmoja wa urais na katika nafasi
za ubunge na udiwani kama vilivyokubaliana, ikiwa ni mara ya kwanza
tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Maandalizi ya uchaguzi huo yanaanza mwezi huu kwa
wapigakura kuandikishwa upya katika Daftari la Kudumu la Wapigakura,
ambalo tangu mwaka 2009 halijawahi kuboreshwa na hivyo kusababisha wengi
kushindwa kupiga kura katika uchaguzi wowote uliofanyika baada ya 2010.
Pengine jambo ambalo linasubiriwa kwa hamu na
wananchi ukiacha Uchaguzi Mkuu na Katiba Mpya ambayo kampeni zake
zitaanza Aprili 30, ni mchakato wa ndani ya vyama vya siasa wa kupata
wagombea urais, hasa kutokana na mvutano ulioanza kujitokeza ndani ya
CCM na mvutano unaotarajiwa ndani ya Ukawa.
Matukio
Tukio litakaloanza mwaka huu ni lile la Januari 30
la uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ambao
utakamilika Aprili 28 ukifanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kulingana na uandikishaji wa majaribio uliofanyika
katika majimbo matatu ya Kawe, Kilombero na Katavi, shughuli yenyewe
inatarajiwa kuvuta hisia na hamasa za Watanzania wengi hasa kutokana na
muda, matatizo ya kukwama kwa mashine za kielektroniki (BVR) na wingi wa
watu waliojitokeza.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ametangaza tarehe ya upigaji Kura ya Maoni kuwa ni Aprili 30.
Februari mwaka huu, CCM imeahidi kutoa msimamo
wake kuhusu wanachama wake walioanza kufanya kampeni mapema kujihusisha
na vitendo vilivyokiuka maadili ndani ya chama na jamii.
Huenda chama hicho kikawaengua baadhi yao kwa kuongeza muda wa onyo hivyo kujikuta wakishindwa kuwania nafasi hiyo, iwapo watabainika kuendelea kukiuka maadili ya chama, licha ya awali kuonywa na kupewa adhabu ya kutojihusisha na masuala hayo mpaka baada ya miezi 12.
Huenda chama hicho kikawaengua baadhi yao kwa kuongeza muda wa onyo hivyo kujikuta wakishindwa kuwania nafasi hiyo, iwapo watabainika kuendelea kukiuka maadili ya chama, licha ya awali kuonywa na kupewa adhabu ya kutojihusisha na masuala hayo mpaka baada ya miezi 12.
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa; Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; mawaziri
Bernard Membe (Mambo ya Nje), Stephen Wasira (Ofisi ya Rais, Uhusiano na
Uratibu), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January
Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Mei utakuwa na tukio la aina yake pale Ukawa na CCM pamoja na
vyama vingine vitakapokuwa vikiteua wagombea urais, ikiwa ni baada ya
wengi waliojitokeza kuchujwa katika vikao vya ndani vya vyama hivyo.
Juni mwaka huu, Rais Kikwete atalivunja Bunge
baada ya kumalizika kwa Mkutano la Bajeti utakaoanza Aprili mwaka huu,
ukiwa tayari umepitisha bajeti ya Serikali ambayo sehemu yake itatumiwa
na Serikali mpya ya awamu ya tano.
Pamoja na kwamba siyo utaratibu wa kikanuni, lakini kwa utamaduni wa Bunge la Tanzania, Rais Kikwete anaweza kutoa hotuba ya kulivunja Bunge.
Pamoja na kwamba siyo utaratibu wa kikanuni, lakini kwa utamaduni wa Bunge la Tanzania, Rais Kikwete anaweza kutoa hotuba ya kulivunja Bunge.
Miezi inayotarajiwa kuwa na changamoto kubwa ni
kuanzia Julai hadi Oktoba ambayo itakuwa ya kampeni za uchaguzi ambao
wagombea urais, ubunge na udiwani watakuwa wakinadi sera zao.
Mwishoni mwa Oktoba, ndipo utakapofanyika Uchaguzi
Mkuu na Tanzania kupata rais mpya ambaye mpaka sasa ni vigumu kutabiri
atakuwa nani na atatoka chama gani.
Hali hiyo inatokana na CCM hadi sasa kuwa na makada zaidi ya 14 wanaotajwa kuutaka urais wakiwamo wanne ambao tayari wametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo.
Kwa upinzani, viongozi wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD vinavyounda Ukawa ndiyo wanaopewa nafasi za kugombea nafasi hiyo. Hao ni Profesa Ibrahim Lipumba, Dk Willbrod Slaa, James Mbatia na Freeman Mbowe huku vyama vyenyewe vikisema vinaweza hata kumpata mtu nje ya muungano huo.
Hali hiyo inatokana na CCM hadi sasa kuwa na makada zaidi ya 14 wanaotajwa kuutaka urais wakiwamo wanne ambao tayari wametangaza nia ya kugombea nafasi hiyo.
Kwa upinzani, viongozi wa vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD vinavyounda Ukawa ndiyo wanaopewa nafasi za kugombea nafasi hiyo. Hao ni Profesa Ibrahim Lipumba, Dk Willbrod Slaa, James Mbatia na Freeman Mbowe huku vyama vyenyewe vikisema vinaweza hata kumpata mtu nje ya muungano huo.
Uchambuzi wa kisomi
Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es
Salaam (Tudarco), Lois- Singa Metili alisema mwaka 2015 ni kipindi cha
mpito ambacho endapo mambo yote yaliyopangwa yatakwenda sawa, miaka
inayofuata itakuwa mizuri kwa Watanzania.
“Hatujui kura za hapana au za ndiyo kwenye Kura za
Maoni ya Katiba zitakuwa ngapi, hatujui kama NEC itapewa meno ya
kutosha ya kusimamia uchaguzi ili tupate rais kwa njia ya haki.”
Alisisitiza kuwa iwapo haki itatumika katika
kupitisha mambo hayo, nchi itajenga msingi imara kwa maendeleo ya watu
wake kwa miaka mingi ijayo.
Alisema kwa kuwa Tanzania mwaka 2014 ilitajwa
vibaya kwenye vyombo vya habari vya Magharibi, ikihusishwa na kashfa za
rushwa, inabidi taasisi zote nchini kurekebisha kasoro hiyo.
Kuhusu siasa, Metili alisema CCM itakuwa na
kibarua cha kumpata mgombea mwenye sifa atakayekubalika kwa wananchi.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema kutokana na mwaka 2015 kukabiliwa na mambo mazito ya kitaifa yanayohitaji fedha nyingi, Serikali itakuwa katika wakati mgumu kifedha.
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema kutokana na mwaka 2015 kukabiliwa na mambo mazito ya kitaifa yanayohitaji fedha nyingi, Serikali itakuwa katika wakati mgumu kifedha.
Dk Ngowi aliutaja mwaka huu kuwa ni wa kipekee kwa
kuwa licha ya kuhitaji fedha nyingi, utaongezewa maumivu na hatua ya
wahisani kukataa kutoa msaada kwa sababu ya kashfa ya escrow iliyotokea
mwishoni mwa 2014.
Alieleza kuwa ingawa maisha ya wananchi yanaweza
yasibadilike sana, lakini Serikali itahitaji kujipanga upya katika
kukusanya fedha.
Uchambuzi wa Dk Ngowi unaungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kusini
(NCCR-Mageuzi), David Kafulila aliyesema mwaka huu uchumi wa nchi
utaporomoka kwa sababu ipo katika mahitaji makubwa ya fedha za uchaguzi,
uandikishaji Vitambulisho vya Taifa na vya kupigia kura sambamba na
upigaji wa kura ya maoni kupitisha Katiba Mpya.
“Uchumi unakua lakini maendeleo ya uchumi
hayaonekani kwa sababu ya matumizi mabaya ya fedha za umma pamoja na
uchumi kukuzwa na sekta za madini, utalii, mawasiliano ambazo hazibebi
watu wengi kama ilivyo katika kilimo, mifugo na uvuvi,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema licha ya mwaka huu
kuwa na mambo mengi muhimu, Serikali haionekani kuchukua hatua za
dharura.
Dk Kijo- Bisimba alisema ili taratibu ziende kama
zilivyopangwa, ilitakiwa hadi sasa nakala za Katiba Inayopendekezwa ziwe
zimeshasambazwa kwa wananchi, lakini hilo linaonekana kusuasua.
“Maboresho ya Daftari la Wapigakura yalitakiwa
yawe tayari, lakini mamlaka hazijajipanga kama ulivyoona kwenye uchaguzi
wa Serikali za Mitaa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema Watanzania wanaingia mwaka
mpya wakiwa wamechanganyikiwa, hawajui nani anasema ukweli kuhusu fedha
za escrow kama zilikuwa ni za umma au la... “Bunge lilisema fedha zile
ni za umma, lakini huyu mwingine naye kasema siyo fedha za umma.”Mkuu wa
Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam (Duce), Dk Aneth Komba alisema;
“Ninachokiona mwaka huu utakuwa mfupi sana kutokana na mambo kuwa
mengi.”
JK atoa salamu za mwisho za mwaka akiwa Rais
Rais Jakaya Kikwete jana alitoa salamu zake za
Mwaka Mpya kwa mara ya mwisho katika utawala wake huku akisema mwakani
atakuwa akifuatilia salamu kama hizo kupitia televisheni na redio akiwa
kijijini kwake Msoga mkoani Pwani.
Katika hotuba hiyo yenye maneno 5,988 iliyojaa
mapitio ya mambo mbalimbali ya mwaka 2014, Rais Kikwete alisema wakati
Rais wa awamu ya tano akitoa zake za kwanza za mwaka mpya, yeye atakuwa
raia wa kawaida na itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa.
Sanjari na hayo, Rais aliwaagiza viongozi wa
Serikali wanaowawekea vikwazo wafanyabiashara wanaouza mazao nchi za nje
kuacha vitendo hivyo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kutimiza azma
yao.
Alisema uzalishaji mazao mwaka huu umeongezeka
hadi tani milioni 16.2 ukilinganisha na tani milioni 14.38 za mwaka 2013
na kwamba Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) si mnunuzi wa
mazao yote hayo, hivyo mengine yatanunuliwa na wafanyabishara
wanaotakiwa kushawishiwa kuyanunua kwa wingi.
“Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni kwamba
pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia njia
halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna
sababu ya kufanya hivyo,” alisema Rais Kikwete.
Aliwataka Watanzania kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la
Wapigakura kwani kushindwa kufanya hivyo kutawanyima fursa ya kupiga
kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa pamoja na Uchaguzi Mkuu.