Imeelezwa kuwa wabunge wengi wamekosa
hofu ya mungu kutokana na kuendekeza waganga wa jadi hivyo kutawaliwa na roho
za kishetani na kuendekeza pesa matokeo yake hawako karibu na wananchi wao.
Hayo yamesemwa na Askofu wa Kanisa la Tanzania Field
Evangelism(TFE)maarufu kanisa la Emmanuel mjini Shinyanga Edson Mwombeki wakati
wa kongamano la siku 5 la wachungaji na maaskofu 200 kutoka makanisa ya
kipentekoste nchini la kufunga mwaka 2014 na kukaribisha mwaka 2015.
Askofu huyo alisema hivi sasa wabunge wanapotoka
bungeni wanaanza kugawa pesa kama andazi na kwamba hakuna mbunge anayetoka
bungeni na kwenda kwa wachungaji kuombewa na badala yake wabunge wamekuwa na
waganga wa kienyeji wakiamini kuwa ndiyo watawasaidia katika uongozi wao na maisha yao kwa ujumla.
“Tumewafanyia uchunguzi,ni wabunge wachache hawana
waganga wa kienyeji,sasa hivi kila mmoja ana waganga wake,wanategemea waganga
wa kienyeji kila saa,sisi ndiyo waangalizi wa watu,tukikujua una ndumba
tunakusalimisha kwa Yesu unaokoka”,alisema Mwombeki.
“Wabunge wanaendekeza uganga wa kienyeji,ndiyo
wanaowazunguka, ndiyo maana maaskofu tumechukia, na sisi biblia inatukaza
kuongozwa na mtu anategemea miungu sasa sisi tunamuuliza katibu mkuu wa CCM
taifa Abdulrahman Kinana,Je CCM ni ya uganga wa kienyeji?”,alihoji Mwombeki.
Aidha alisema
Chama cha Mapinduzi kimeanguka katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2014 kwa
sababu mbalimbali ikiwemo wakuu wa wilaya na mikoa kutokuwa karibu na wananchi
na wabunge kutumia pesa zao kuhonga
wananchi na sasa wengine wanadiriki hata kununua hadi viwanja vya makanisa ili
wajenge gereji zao.
“Leo nataka nimwambie ndugu yangu Kinana anayefanya
kazi kubwa kuimarisha chama kuwa mchawi wa CCM ni baadhi ya watendaji
wake,asiposahihisha ategemee anguko kubwa katika uchaguzi mkuu 2015,na hawa wabunge
wasimdanganye”,alisema askofu huyo.
“Tunampa
tahadhari tu Katibu mkuu wa CCM Kinana na hii siyo siasa kwa sababu hii ishara
ya kuanguka kwenye vijiji inatosha,afanye jitihada aite wachungaji kama anaweza
kuwasikiliza,na akumbuke kuwa hawa wabunge, aliowaweka kuwaongoza wananchi
hawasikilizi watu watamdanganya tu”,aliongeza Mwombeki.
Askofu Mwombeki alimshauri Kinana kurekebisha changamoto
zinazotokana na viongozi wake wabovu ili kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi
ujao huku akimtaka kuacha kukaa ofisini na kupokea taarifa kwa sababu atadanganywa
bali atembelee wananchi.
Aidha alimshauri Kinana kushughulika na watenda kazi
wake badala ya kung’ang’ana na wala rushwa pekee huku akimtaka kufuatilia
katika mikoa waliyoanguka tatizo siyo sakata la Tegeta Escrow bali uongozi
mbovu wa wakuu wa wilaya,wakuu wa mikoa na wabunge wasiopenda kuwajibika na
kutokuwa karibu na wananchi.
Alisema katika uchaguzi mkuu ujao wachungaji na
maaskofu hawataki wabunge wafanyabiashara wanaolangua wananchi na badala yake wanajipanga
kupeleka wabunge wenye hofu ya mungu ili waweze kumsaidia rais ajaye.
“Tunataka viongozi wenye hofu ya mungu,wenye nia ya
kusaidia nchi na kusaidia kupumua kwa rais ajaye,kwani rais wetu wa sasa Jakaya
Kikwete ametumia nguvu nyingi kwa watu wabovu,Tunampongeza kwa kazi nzuri,rais
huyu kila mara matatizo,huwezi kuongoza nchi kwenye matatizo unamaliza hili
linakuja jingine”,alisema.
Aidha alisema alishangaa kuona wagombea wa CCM katika
uchaguzi wa serikali za mitaa waliokuwa wakifanya kampeni kwa kutumia magari na
wengine wakiwa wamevaa suti wakishindwa na wagombea wa vyama vya upinzani wenye
hali duni ya kimaisha ambao vazi lao kuu ni kandambili hali inayoonesha kuwa
wananchi hawaridhishwi na utenda kazi wa viongozi waliowachagua.
Aliongeza kuwa viongozi wengi wa vyama vya upinzani
walioshinda katika uchaguzi walianzia makanisani kuombewa ndiyo maana
wameshinda bila kutumia pesa na nguvu nyingi.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin