Diwani wa kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga,
Sungura George (mwenye shati la pundamilia)aliyepita jirani na ofisi hizo za CCM akitokea ofisi za afya za
manispaa ya Shinyanga akisukumwa na Vijana wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini baada ya kuvamiwa ghafla na
vijana hao na kushambuliwa kwa kuchapwa makofi-picha na Marco Maduhu-Malunde1 blog
Mzimu wa Uchaguzi wa serikali za mitaa Tanzania umeendelea kuitesa CCM
mkoani Shinyanga ambapo katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya vijana wa
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Shinyanga mjini wamefunga kwa saa kadhaa ofisi
ya CCM wilayani humo wakishinikiza kuondolewa kazini kwa katibu wa wilaya hiyo Charles
Sangula.
Tukio hilo limetokea jana saa tatu asubuhi katika ofisi za CCm wilaya ya
Shinyanga mjini ambapo mbali ya kumkataa katibu huyo pia vijana hao zaidi ya 20
waliwakataa katibu mwenezi wa wilaya, Charles Shigino na mchumi wa wilaya,
Ahmed Mapalala wakidai kuwa sio waadilifu na wanawadharau UVCCM.
Inaelezwa kuwa viongozi hao wanawatuhumiwa kuchangia kushindwa kwa wagombea
wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika kote Desemba 14,mwaka
huu.
Vijana hao wamemuomba mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete na katibu
mkuu, Abdulrahman Kinana wachukue hatua mara moja za kuwaondoa madarakani
watendaji hao wanaodaiwa kufanya mikakati michafu ya kutaka kukiuza chama hicho
na kwamba kitendo chao kinaweza kuleta madhara makubwa katika uchaguzi mkuu wa
mwezi Oktoba mwaka huu.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga
mjini vijana hao walidai hatua yao ya kuwakataa viongozi hao wakuu wa wilaya
inatokana na kupata ushahidi kwamba kushindwa kwa CCM katika mitaa mingi
manispaa ya Shinyanga walihusika kwa njia moja ama nyingine.
Walisema hata hivyo viongozi hao wamekuwa hawatoi ushirikiano kwao (UVCCM)
na mara nyingi huwadharau na kutowathamini pamoja na kwamba mchango wao ndani
ya chama ni mkubwa lakini hawapewi ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi
hao hali iliyochangia CCM kupoteza mitaa mingi katika manispaa ya Shinyanga.
Mmoja wa vijana hao Samwel Jackson mkazi wa kata ya Masekelo manispaa ya
Shinyanga alisema waliamua kufunga ofisi hizo kwa lengo la kuwazuia katibu wa
CCM wilaya, mwenezi wake na mchumi wa wilaya wasiingie ofisini baada ya
kuchoshwa na vitendo vyao vinavyoashiria usaliti ndani ya chama.
“Tumechukua hatua hii kwa nia nzuri tu, vijana tumefanya uchunguzi wetu na
kubaini kuwa wenzetu hawa walihusika kwa njia moja ama nyingine kuchangia
kushindwa kwa wagombea wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa manispaa ya
Shinyanga ambapo wagombea wengi wa CHADEMA walishinda katika mitaa mingi”,alieleza
Jackson.
“Katibu wa CCM wa wilaya,mara kwa mara amekuwa akitudharau na wakati
mwingine huwashusha vijana katika gari lake kwa madai ya kutowatambua hali
ambayo imekuwa ikituvunja moyo, tuna mapenzi makubwa na CCM,hatuoni sababu ya kujitoa
badala yake viongozi hawa ndiyo
waondolewe”,aliongeza Jackson.
Hata hivyo kwa wakizungumza na waandishi wa habari
kwa nyakati tofauti watuhumiwa hao,
ambao wamedaiwa kuwadharau vijana hao wa CCM,pamoja na kukihujumu chama,
walikanusha tuhuma hizo na kudai hazina ukweli wowote, isipokuwa vijana hao
wana lao jambo, huku wakihofia kuwa kuna mtu fulani kawapandikiza ili kukichafua
Chama.
MWENYEKITI WA CCM AZUNGUMZA
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Kanali mstaafu
Tajiri Maulid aliyefika katika ofisi hizo baada ya kupata taarifa, aliwasihi
vijana hao wafuate utaratibu kwa kuandika barua na kuwasilisha malalamiko yao
ili yaweze kufanyiwa kazi ambapo pia aliwaomba waruhusu kufunguliwa kwa ofisi
ili kazi ziweze kufanyika.
Kanali Maulid alisema haitokuwa rahisi kwa malalamiko yao kufanyiwa kazi
iwapo ofisi hizo zitaendelea kufungwa na kwamba kulalamika kwa mdomo bila ya
maandishi hakuna maana yoyote na kuwasihi waandike barua itakayojadiliwa katika
vikao husika na kutolewa maamuzi.
“Andikeni barua na mueleze ni mambo gani mnayotaka yafanyiwe kazi,
kumbukeni mambo ya chama hayatolewi maamuzi na mtu mmoja bali kinachofanyiwa
kazi ni maamuzi ya vikao, tumepokea malalamiko yenu, fungueni mlango” ,alieleza
Kanali Maulid.
Baada ya ushauri wa mwenyekiti huyo wa wilaya vijana hao walikubali
kufungua ofisi hizo mnamo saa 3.50 asubuhi ambapo pia walikusanyana na kuanza
hatua ya kuandika barua waliyoshauriwa kuiandika itakayoelezea malalamiko yao
yote ikiwemo kupendekeza kuondolewa madarakani kwa viongozi wanaowakataa.
DIWANI WA CHADEMA APIGWA VIBAO
Katika sekeseke hilo diwani wa kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga, Sungura
George aliyepita jirani na ofisi hizo za CCM akitokea ofisi za afya za manispaa
ya Shinyanga alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuvamiwa ghafla na vijana
hao na kumshambulia kwa kumchapa makofi matatu huku akitakiwa kupotea katika eneo
hilo mara moja huku akinusurika kugongwa na gari.
Kwa upande wake diwani wa CHADEMA kata ya Ndala, Sungura George alisema
kufuatia kitendo cha kushambuliwa kwa kipigo na vijana hao wa CCM anakusudia
kwenda kuwashtaki polisi ili sheria iweze kuchukua mkondo wake baada ya kuvamiwa
na kupigwa bila sababu zozote alipokuwa akipita barabarani.
MGOGORO
NDANI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI
Tukio la vijana wa CCM linakuja siku chache tu baada
ya viongozi wa CCM kufikia hatua ya kutukanana matusi ya nguoni kutokana na
kushindwa kufanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika manispaa
ya Shinyanga.
Desemba 15,2014 majira ya saa 5 na nusu asubuhi,katibu
wa Siasa na uenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Charles Shigino na katibu
wa umoja wa Vijana wilaya ya Shinyanga Mjini (UVCCM), Zawadi Husein Nyambo
walitukanana matusi ya nguoni almanusura wachapane makonde wakati Shigino
akiingia katika ofisi za Chama, (mlangoni).
Inaelezwa kuwa wakati Shigino akiingia katika ofisi za
chama ghafla alitokea katibu wa umoja wa vijana (UVCCM), Zawadi Hussein Nyambo,
na kumzuia kuingia katika ofisi hizo,na kuanza kumrushia maneno machafu hali
iliyosababisha mtafaruku mkubwa na kujaza umati wa watu.
Alisimulia mkasa uliompata kwa waandishi wa habari Shigino alisema ugomvi
huo ulikuja baada ya chama chake kufanya vibaya katika kata ya Ngokolo ambapo
wapinzani wao Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema kupata ushindi
katika mitaa sita huku CCM, wakiambulia mtaa mmoja pekee huku
mwanaCCM huyo akimtuhumu kuwa yeye ndiye kasababisha matokeo hayo kuwa mabovu.
Katibu huyo wa umoja wa Vijana wilaya ya Shinyanga
Mjini (UVCCM), Zawadi Hussein Nyambo alisema alimzuia katibu mwenezi huyo
kuingia katika ofisi za chama hicho kwa madai kuwa yeye ni msaliti wa chama na
amekuwa akitoa siri na kuzipeleka kwa wapinzani.
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika
Desemba 14,2014, kati ya mitaa 55 katika wilaya ya Shinyanga Mjini, CCM,
walipata ushindi katika mitaa 26 huku (CHADEMA) wakipata mitaa 29, na katika
kata ya Ngokolo yenye mitaa 7, CHADEMA walipata mitaa 6 huku CCM wakiambulia
mtaa mmoja pekee, matokeo ambayo yamesababisha ugomvi ndani ya (CCM) wakisaka
mchawi wao.
|
Social Plugin