Wachimbaji watatu wa madini ya dhahabu ya Kalole kata ya
Lunguya wilayani Kahama mkoani Shinyanga
wamefariki dunia baada ya kufukiwa na udongo wakiwa kwenye shimo la
dhahabu wakitafuta dhahabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa
Shinyanga Justus Kamugisha alisema tukio hilo limetokea Januari 7,2015 saa 12
asubuhi katika machimbo madogo ya dhahabu ya Kalole kata ya Lunguya,tarafa ya
Msalala wilayani Kahama.
Aliwataja waliofariki kwa kufukiwa kwenye shimo hilo la dhahabu kuwa ni Kulwa Magele(20) mkazi wa Shishani wilaya ya
Bariadi mkoani Simiyu, Ihalu Maheme(23) mkazi wa Idisa wilaya ya Bariadi mkoani
Simiyu na Lameck Frank(22) mkazi wa Nzega mkoani Tabora.
Kamanda Kamugisha alisema vijana hao ambao ni wachimbaji
wadogo wa madini waligundulika wakiwa wamekufa ndani ya shimo la kuchimbia
dhahabu na inaelezwa kuwa waliingia kwenye shimo hilo ambalo halitumiki kwa nia
ya kuchimba dhahabu ndpo likabomoka na kuwafukia na kusababisha vifo vyao papo hapo.
Wakati huo huo mwanamke aitwaye Sayi Shitunguru(50)
mkazi wa kijiji cha Buruma kata ya Isaka
wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ameuawa kwa kupigwa kitu kizito kichwani na
watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake.
Kamanda Kamugisha alisema tukio hilo limetokea Januari
7,2015 saa 1 asubuhi ambapo mwanamke huyo akiwa nyumbani kwake alivamiwa na
mtu/watu wasiojulikana kasha kumpiga na kitu kizito kichwani na kusababisha
kifo chake papo hapo.
Alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na jeshi la polisi linaendelea kufanyan
uchunguzi ili kubaini chanzo chake.
Hata hiyvyo alisema tayari wanamshikilia mtu mmoja
aitwaye John Jota(33) mkazi wa Kazungu
wilayani Kahama kwa mahojiano zaidi huku akiwataka wananchi kushirikiana na
polisi ili kusaidia kukamatwa kwa wahusika wa mauaji hayo.
Na Kadama Malunde-Kahama