Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linawasaka walinzi wawili
wa kampuni ya Prosper Security Guard kwa kosa na kuvunja ofisi ya Jambo Oil
Mill and Ginnery Limited kisha kuiba fedha shilingi milioni 1,070,000/= na
kutoweka na bunduki mbili aina ya Shortgun na risasi 7.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari,kamanda wa polisi mkoa
wa Shinyanga Justus Kamugisha(pichani) alisema tukio hilo limetokea Januari 9,2015 saa
moja asubuhi katika eneo la mtaa wa Ibadakuli kata ya Ibadakuli manispaa ya
Shinyanga.
Kamanda huyo alisema siku hiyo mkurugenzi wa Jambo Ginnery
Mohamed Hawadhi(48) aligundua ofisi ya kampuni imevunjwa na kuibwa fedha taslim
shilingi 1,070,000/= zilizokuwa ndani ya kasiki la chuma mali ya kampuni hiyo.
Kamanda Kamugisha aliongeza kuwa katika tukio hilo walinzi
wawili wa kampuni ya ulinzi ya Prosper Security Guard waliokuwa wakilinda ofisi
hiyo walitoweka na bunduki mbili aina ya Shortgun zenye namba F658126 na R65967
pamoja na risasi 7.
Aliwataja walinzi hao kuwa ni William Ubogo na Eliamani
Simoni ambao bado wanatafutwa na jeshi
la polisi ili wakikamatwa hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Hata hivyo Kamanda Kamugisha alisema baada ya jeshi la polisi
kupata taarifa juu ya uhalifu huo lilifanya msako mkali na Januari 10,2015 saa
6:00 mchana lilifanikiwa kupata silaha zote mbili na risasi 7 zikiwa
zimetelekezwa katika maficho karibu na kiwanda hicho.
Na Kadama Malunde-Shinyanga