SAKATA la ofisa
mtendaji wa kata ya Nkome Francis Kagoma
kuuza ng’ombe wa wizi kisha kutokomea kusikojulikana limechukua sura
mpya baada ya wananchi kuamua kufunga ofisi yake na kumtaka mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya wilaya ya Geita kupeleka mtendaji mwingine.
Wakizungumza na Malunde1 blog kijijini
hapo huku wakiwa wamefura hasira wananchi hao walidai
kuwa,wamefikia hatua hiyo ya kufunga ofisi kama salamu kwa mwajiri wake kuwa
hawahitaji kuongozwa na kiongozi mwizi.
Tukio la wananchi
kufunga ofisi limetokea jana majira ya jioni baada ya kuona uongozi wa
halmashauri hiyo haujachukua hatua dhidi ya mtendaji huyo mbali na kutoa kilio
cha mara kwa mara kuhusu mtendaji Kagoma ambaye mbali na tukio la wizi wa ng’ombe
wamekuwa wakimlalamikia kwa kutafuna fedha za miradi ya maendeleo.
‘’Tumechoka kuongozwa
na mwizi na hii ni salamu kwa mwajiri wake kwamba wananchi wa kata ya Nkome
tumechoshwa na uongozi wa kifisadi,tumeshamlalamikia huyu mtendaji mara kwa
mara na mkurugenzi anajua lakini hatuoni hatua zinazochukuliwa dhidi yake na
sasa ameuza ng’ombe wa wizi na kukimbia tumefunga ofisi yetu na tunamuomba
mkurugenzi atuletee mtendaji mwingine’’Alisikika mmoja wa wananchi hao ambaye
jina lake halikupatikana mara moja.
Hivi karibuni kigogo
huyo wa halmashauri ya wilaya ya Geita ambaye ni mtendaji wa kata ya nkome
Wilaya na mkoa wa Geita,Peter Francis Kagoma aliikimbia kata yake baada ya
kudaiwa kuuza ng’ombe wa wizi kwa thamani ya Tshs 350,000.
Kutokana na hali
hiyo,jeshi la polisi Wilaya ya Geita lililazimika kumshikilia Mashauri
Magoti(54),mkazi wa kijiji cha Ihumilo kilichopo katika kata hiyo ambaye
inaelezwa alishirikiana na mtendaji huyo kumuuza ng’ombe huyo.
Kwa sasa ng’ombe huyo
amekamatwa na analindwa na polisi wa kituo kidogo cha polisi Nkome hadi hapo
mtuhumiwa namba moja ambaye ni mtendaji atakapopatikana na kufikishwa
mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Mwenyekiti wa
kitongoji cha Ihumilo ilipoibiwa ng’ombe hiyo Thomas Alila alisema,Desemba 13 walikuta ng’ombe huyo akiwa ametelekezwa na mtu
asiyejulikana nje ya nyumba ya Mashauri Magoti huku akiwa amefungwa kamba
kwenye mti.
Amesema walimchukuwa
ng’ombe huyo hadi ofisi ya Mtendaji wa kata ya Nkome ambako walimkabidhi kwa
Weo Kagoma na mbele ya mtendaji wa kijiji Charles Buligi kwa lengo la
kumtangaza kama utaratibu wa kisheria unavyoelekeza.
Hata hivyo katika
hali isiyotarajiwa,Desemba 23 mwaka huu ofisa mtendaji huyo,alimuuza ng’ombe
huyo kwa thamani ya Tshs 350,000/=,na baadaye ng’ombe huyo alikamatwa na
wananchi akiwa mbioni kuchinjwa.
Akizungumzia hali
hiyo kabla ya kukamatwa,mchungaji wa ng’ombe huyo Magoti ambaye kwa sasa
anashikiliwa na polisi,alikiri mtendaji Kagoma kumuuza ng’ombe huyo nayeye
kupatiwa mgao wa Tshs 100,000 kama malipo ya kumlinda ng’ombe huyo kuanzia
alipokutwa ametelekezwa nyumbani kwake hadi siku ya kuuzwa.
Naye Kagoma
alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi simu iliita bila kupokelewa.
Mkuu wa kituo cha
polisi cha Nkome D/CPL Gwaga Mtawa ambali na kukiri mtendaji huyo
kukimbia na ng’ombe huyo kushikiliwa kituoni hapo alimtaka mwandishi wa habari
hizi kumtafuta kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo ambaye ndiye
msemaji mkuu wa jeshi hili.
Mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Ali Kidwaka alikiri kuwepo kwa mkasa huo
dhidi ya mtendaji huyo ambapo yeye ni mwajiri wake na kuahidi kuchukuwa hatua
sitahiki.
Na Victor Bariety-Malunde1 blog Geita
Social Plugin