Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Joseph Konyo |
Wananchi katika kisiwa cha Izumacheli Kata ya Nkome Wilayani
Geita mkoani Geita, wamefanikiwa kumuua mtuhumiwa wa ujambazi akiwa na SMG
yenye risasi 28, kwa kumshambulia na mawe pamoja na marungu kisha mwili wake
kuuteketeza kwa moto hadi ukawa majivu.
Mtuhumiwa huyo,alikamatwa akijiandaa kufanya uharifu kwenye
kisiwa hicho akiwa na silaha hiyo ya
aina ya SMG na Risasi 28 iliyofutwa namba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo, alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kumtaja aliyeuawa kuwa ni Mawazo Nagabona(43)mkazi wa
kisiwa cha Ikuza Wilayani Mreba Mkoani Kagera.
Alisema tukio hilo lilitokeajana saa 11 alfajiri baada
ya wananchi wa kisiwa hicho kupata taarifa kwamba mtuhumiwa na wenzake ambao
hawajakamatwa wamepanga kufanya uharifu kwenye kisiwa hicho kwa kuwapora
wafanyabiashara na wavuvi wa kisiwa hicho mali zao.
Hata hivyo kamanda Konyo alifafanua kuwa,wananchi hao
walifanikisha kubaini hilo kutokana na mafunzo ya polisi jamii waliyoyapata na kuwajengea uwezo wa kutambua
waharifu na namna ya kupashana habari namna ya kuchukuwa hatua kwenye matukio
ya dharula kama hilo.
“Baada ya kupata taarifa za majambazi hao wananchi hao walianza kumzingira na baadaye jambazi huyo
aliwapeleka ilipo Bunduki yake aliyokuwa ameihifadhi kwenye mtumbwi na ndipo
walipochukuwa jukumu la kumshambulia kwa mawe na malungu kisha kumchoma moto kabla ya polisi kufika na kumkuta akiwa ameteketea
kwa moto na kubaki majivu’’ alisema Kamanda Konyo.
Aliongeza kuwa,iwapo jeshi la polisi lingekuwa na boti yake
lingewahi eneo la tukio kabla ya mtuhumiwa huyo kuuawa na lilichelewa kutokana
na mazingira ya kufika eneo hilo kuwa magumu na hatarishi na kuwataka wananchi
kuacha kujichukulia sheria mkononi
wanapokuwa wamefanikiwa kuwadhibiti waharifu na badala yake wawafikishe
kwenye vyombo vya dola.
‘’Haki ya kuishi ni haki ya kikatiba na inapotokea wananchi
wamemuua mtuhumiwa wanakuwa wamepunguza tatizo kidogo maana wanafanya kazi ya
kuwapata wenzake kuwa ngumu lakini kama mtuhumiwa akiwepo atawataja
anaoshilikiana nao na inakuwa kazi rahisi kukamata mtandao wake’’alisema Konyo.
Hili ni tukio la pili kutokea katika kipindi cha miezi 6
iliyopita ambapo Juni 24 mwaka jana watuhumiwa wa ujambazi walizua taharuki
mjini Geita baada ya kuvamia mchana
kweupe kwenye duka la mfanyabiashara wa bia la Blue Coast Investment,
linalomilikiwa na Ignas Athanas na kupora fedha kisha kuondoka baada ya kupiga
risasi moja hewani, kuwatisha watu.
Baada ya hapo, walivamia katika duka la wakala wa kampuni za
simu, ambapo yalipora fedha na kumuuwa kwa risasi mmiliki wa duka hilo Gosbert
Kulwa (59), maarufu kwa jina la Warwa. Pia walimpora bastola na baadaye
majambazi hao waliuawa na wanafunzi wa shule ya Sekondari Nyang’hwale Mkoani
Geita wakati wakijaribu kutoroka wakitumia pikipiki aina ya Sun LG yenye namba
T460 CVQ, yaliyoondoka nayo kwa kasi
huku yakinusurika kugongwa na basi la Sabuni lililokuwa likitokea Mwanza kwenda
Mganza, wilayani Chato.
Wakati wa tukio hilo, shughuli zilisimama kwa muda katika mji wa Geita, huku watu wakikimbia ovyo kuokoa maisha yao kabla ya polisi kufika na kuanza kuyafuatilia kabla ya kukuta wanafunzi hao wamekwishayaua na kufanikiwa kuokoa bastora yaliyopora pamoja na SMG waliyokuwa wakiitumia.
Na Victor Robert-Malunde1 blog Geita