Mahakama
ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Nzega mkoani Tabora imemhukumu kifungo cha
maisha Kashindje Shija (50), baada ya kupatikana na kosa la kumbaka
mtoto mwenye umri wa miaka mitano.
Akisoma
hukumu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya
Nzega Joseph Ngomero, alisema kuwa, kutokana na ushahidi uliotolewa
mahakamani hapo, amelazimika kutoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa watu
wengine wanaokusudia kufanya vitendo kama hivyo.
Hakimu
Ngomero aliongeza kwa kusema kuwa, kutokana na kitendo cha kinyama
alichokifanya Shija cha kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 5, mahakama
hiyo imelazimika kumhukumu kifungo cha maisha jela.
Awali
Mwendesha Mashitaka wa Serikali wilayani Nzega Melito Ukongoji
aliiambia mahakama hiyo kuwa, mnamo Mei 19, 2014 katika Kijiji cha
Kidete wilayani Nzega saa 8 mchana, Shija alifumaniwa chini ya mti wa
mwembe akiwa anambaka mtoto huyo.
Aidha
Melito aliongeza kuwa kutokana na kitendo alichokifanya mtuhumiwa
kilimsababishia mtoto huyo maumivu makali katika mwili wake pamoja na
kutoka damu nyingi.
Mwendesha
Mashitaka huyo, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe
fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo kutokana na kitendo
kilichofanywa na mtuhumiwa cha kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 5.
Kabla
ya hukumu hiyo kutolewa, mahakama hiyo ilitoa nafasi ya utetezi kwa
mtuhumiwa ambapo aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu kutokana na
kuwa mwathirika wa virusi vya Ukimwi.
Social Plugin