Akina mama wakiwa eneo nje ya ofisi wakishuhudia katibu wa CUF wilaya ya Shinyanga mjini akiwarushia maneno machafu waandishi wa habari waliofika eneo hilo kutimiza wajibu wao,ambapo pia akiwa na viongozi wenzake waliwatishia kuwapiga na kuwavunjia kamera zao na kuwataka waondoke eneo hilo kwani malalamiko ya akina mama hayo hayawahusu waandishi wa habari |
Wa kwanza kushoto ni katibu wa CUF wilaya ya Shinyanga mjini Said Sizya akitukana waandishi wa habari( hawako pichani)
Akina baba hawakuwa nyuma nao walijisogeza kushuhudia kilichokuwa kinajiri kwenye ofisi hizo za CUF mjini Shinyanga |
Wananchi wakimshangaa katibu huyo kugombana na waandishi wa habari wakati wamekuja kusikiliza malalamiko |
Katibu wa CUF wilaya ya Shinyanga mjini Said Sizya akiendelea kukabiliana na waandishi wa habari walioonesha kutotishika pamoja na kuwepo kwa vitisho vya hapa na pale kutoka kwa viongozi wa CUF |
Aliyenyosha mkono juu(nguo nyeupe) ni mmoja wa viongozi wa CUF ambaye ndiye alikuwa anaandikisha majina ya akinamama sambamba na kuwauzia kadi za CUF kwa shilingi 500 ili wachukue mkopo,naye bila aibu akitukana waandishi wa habari
+++++++++++++++++++++++++
Ofisi
za Chama cha Wananchi CUF wilaya ya Shinyanga Mjini mkoani Shinyanga zimegeuka
uwanja wa matusi baada ya baadhi ya viongozi wake wakiongozwa na katibu wa
wilaya hiyo Said Sizya kutaka kuwapiga na kuwavunjia vifaa vyao vya kazi
waandishi wa habari waliofika katika ofisi za chama hicho kuchukua matukio
baada ya kupewa taarifa kuwa kundi la wanawake zaidi ya 50 limeandamana
katika ofisi hizo wakidai kudhulumiwa pesa walizotoa kwa ajili ya kupatiwa
mkopo.
Waandishi wa
habari waliojikuta wanafanya kazi zao katika mazingira magumu ni Suzy
Butondo wa gazeti la Mwananchi na The Citizen,Kadama Malunde wa gazeti la
Mtanzania na Kahama FM ambaye pia ni Bloga Maarufu kupitia www.malunde1.blogspot.com na Emmanuel Mpanda mwakilishi wa
Zanzibar Television.
Waandishi hao
wa habari walifika katika ofisi za chama hicho jana majira ya saa 10 jioni baada
ya kupewa taarifa kuwa wanawake zaidi ya 50 kutoka maeneo mbalimbali ya
manispaa ya Shinyanga wameandamana wakidai kudhulumiwa pesa walizotoa kwa ajili
ya kupewa mkopo wa fedha na chama hicho.
Walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa wakati waandishi hao wa habari wanafanya mahojiano na wanawake hao nje ya ofisi za chama hicho kujua nini hasa kimewafikisha hapo,ghafla walijitokeza viongozi wa CUF wakiongozwa na katibu wa chama hicho Said Sizya wakiwa wamehamaki kutokana na kile kilichoelezwa kuwa wamevurugwa na akina mama hao.
Walisema viongozi hao wakiongozwa na Sizya
waliwataka waandishi hao wa habari waondoke haraka katika eneo hilo kwa madai
kuwa hawatakiwi kufanya kazi za uandishi katika eneo bila kuwataarifu
viongozi wa chama hicho na kwamba walitakiwa wawaulize kwanza wao kwanini akina
mama hao wapo mahali hapo badala ya kuanza kuzungumza na wananchi moja kwa
moja.
“Ondokeni
haraka sana hapa,mmekuja kufanya nini,nani kawaita,mnataka kuleta vurugu kwa
watu wetu,tutawapiga na tutavunja kamera zenu sasa hivi,hatutaki mpige picha
mahali hapa,haya mambo hayawahusu”,walisikika wakisema viongozi hao wa
CUF,walieleza mashuhuda hao.
“Mmekuja hapa
bila taarifa,hamjafuata utaratibu mlitakiwa muongee na sisi viongozi kwanza
,Ondokeni sitaki kuwaona,hapa ni mahali pangu,sitaki muongee na watu
wangu,sitaki kuzungumza na nyinyi,sitaki hata muingie ofisini kwangu,nendeni
mkatangaze kwenye vyombo vyenu”,alisema Katibu wa CUF huku akiwasukuma
waandishi hao wa habari.
Pamoja vitisho hivyo kutoka kwa viongozi hao wa CUF wakiongozwa na katibu wao,waandishi wa habari hawakusaliti maadili ya kazi yao katika kuihabarisha jamii hivyo kulazimika kufanya kazi katika mazingira magumu ya vitisho vya hapa na pale ikiwemo kukatazwa kupiga picha na kutishiwa kuvunjiwa kamera zao.
Wakizungumza na waandishi wa habari nje ya ofisi hizo akina
mama hao ambao walikuwa na kadi za CUF ikiashiria kuwa ni wanachama wa chama
hicho ,waliuomba uongozi wa Chama hicho kuwapatia mkopo wao kama walivyowaahidi
kuwasaidia kuinua uchumi wao badala ya kutoa ahadi hewa na kuwapa matumani ya
kupata pesa hizo kila siku.
“ Sisi mwezi Desemba 2014 tulitangaziwa na CUF kuwa kuna
mikopo inayotolewa kwa akina mama bila riba ya aina yoyote,kiingilio shilingi
12,500/= na kadi ya CUF unayopaswa kuilipia shilingi 500/= jumla shilingi
13,000/= baada ya hapo wakatuahidi watatupatia mkopo wa shilingi milioni 1.5
kwa kila kikundi cha watu watano tarehe 28,Januari 2015 lakini mpaka sasa
wanatuzungusha tu”,alisema Annastazia Yasin.
“Kilichotuleta hapa, tunalalamikia pesa zetu tarehe 27
Desemba waliahidi kutupatia pesa Januari 28,2015 lakini hadi leo bila bila,
kila siku tunakuja kufuatilia pesa zetu ,tunachohitaji sisi ni mkopo wetu kwani
wengine tumekopa pesa kwa watu ili kujiunga kupata mkopo kwa ajili ya shughuli
mbalimbali ikiwemo ujasiriamali”,Justina Simon.
Kwa upande wake mmoja wa wakazi wa Shinyanga Maganga Ng’wagi
aliyekuwa ameambatana na mke wake Joyce Musa katika ofisi hizo aliwaomba
viongozi wa CUF kutekeleza ahadi zao kwa wakati na kama walivyoahidi kwa mara
nyingine kutoa mikopo hiyo siku ya Jumatano wiki ijayo.
“Ndugu waandishi ,wakati mwingine sisi tuliooa tunapata
wasiwasi kila siku mke wako anaaga kufuata mkopo lakini hauuoni,nini maana yake
sasa,hawa ndugu zetu wajitahidi tu kutekeleza wanayoyasema,sisi hatuna ugomvi
nao,kwani wanataka kutusaidia”,alieleza Ng’wagi.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa Shinyanga walioshuhudia tukio
hilo walieleza kusikitishwa na kitendo cha katibu huyo wa CUF kugeuka mbogo kwa
waandishi wa habari waliofika eneo hilo kutimiza wajibu wao huku wakiongeza
kuwa pengine kuna jambo ka siri katika ofisi hiyo.
Na Mwandishi wetu Shinyanga mjini
Social Plugin