Mauaji Shinyanga!! WATU WATATU WAKUTWA WAMEUAWA NDANI YA NYUMBA, MIILI YAO YAKUTWA IMEHARIBIKA,YUMO MKE WA MGANGA WA KIENYEJI



Habari kutoka kitongoji cha Shatimba, kijiji cha Bugogo kata ya Mwamala tarafa ya Samuye wilaya ya Shinyanga vijijini ni kwamba watu watatu  wamekutwa wameuawa  na miili yao ikiwa imeharibika vibaya huku ikidaiwa huwa huenda watu hao waliuawa zaidi ya siku 5 zilizopita kwa kushambuliwa na watu wasiofahamika kisha kufungiwa ndani ya nyumba.

Malunde1 blog imeambiwa kuwa watu hao,akiwemo mwanamme mmoja,binti na kikongwe anayedaiwa kuwa mganga wa  kienyeji wamekutwa wamekufa ndani ya nyumba  na wameonekana kuwa na majeraha katika miili yao huku kichwa cha bibi  kikionekana kama kimepigwa kwa kitu kizito.

Habari zinasema kuwa miili ya watu hao imekutwa imeharibika vibaya kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali vinavyodhaniwa kuwa mapanga.

Akizungumza na malunde1 blog diwani wa kata ya Mwamala Hamis Mwenda Masanja  amesema miili ya watu hao imegundulika jana saa 11 jioni ambapo watu watatu wakiwemo wageni wawili binti aitwaye Christina Samweli(18) mkazi wa  kitongoji cha Matanda kijiji cha Singita kata ya Usanda na mwanamme mkazi wa Karitu Nzega(hatujapata jina lake) anakadiriwa kuwa na miaka 35-40  na mwenyeji wao bibi  Shija Bundala(80) walikutwa wameuawa ndani ya nyumba.

"Inavyoonekana kulikuwa na vurugu humo ndani iliyosababishwa na wauaji,na huyo mwanamme alikuwa amelala kwenye chumba kingine na wanawake chumba kingine,na pengine mwanamme alipoona kuna vurugu akatoka chumbani na mwili wa mwanamme huyo ulikutwa sebuleni huku miili ya binti na bibi ikiwa kwenye chumba walichokuwa wamelala,diwani huyo aliiambia malunde1 blog. 

Taarifa kutoka eneo la tukio hilo zinasema chanzo cha tukio hilo huenda ikawa ni imani za kishirikina. 

Miili ya watu hao imezikwa leo Jumapili saa tano asubuhi baada ya jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kuruhusu wazikwe.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post