Baraza la maadili ya utumishi wa umma limeshindwa kumuhoji mbunge wa Bariadi Magharibi Mh Endrew Chenge baada kuwasilisha zuio la mahakama kuu lililozua kutokuendelea kujadili miamala ya Escrow huku wanasheria wa sekretarieti ya baraza hilo wakipingana naye kwa madai kuwa wao wanajadili ukiukwaji wa maadili na siyo miamala ya Escrow.
Kufuatia hali hiyo mwenyekiti wa baraza hilo jaji mstaafu Hamisi Msumi ameahirisha kikao hicho hadi Feb 26 mwaka huu ili wajumbe wapate muda wa kupitia zuio hilo ambapo baraza litakuja na uamuzi ama wa kuendelea au kusitisha hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi wa sakata hilo.
Akisoma hati ya malalamiko dhidi ya Chenge, mwanasheria wa sekretarieti ya maadili, Hassan Mayunga amesema mlalamikiwa amekiuka maadili ya viongozi wa umma ambapo akiwa mwanasheria mkuu wa serikali AG mwaka 1995 aliishauri serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na kampuni ya Independent Power Solution Limited IPTL wa kuongeza uzalishaji wa umme.
Aidha ameongeza kuwa wakati anafanya hayo hakuweka wazi kuwa ana maslahi binafsi na baada ya kustaafu wadhifa huo Desemba 2005 aliingia mkataba wa kuwa mshauri mwelekei wa kampuni ya Vip Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na hisa asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL kitendo ambacho ni ukiukwaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujinufaisha na utumishi wake uliopita.
Akitetea hoja yake ya kutaka baraza hilo lisitishe zoezi la kumuhoji Mh Chenge amesema malalamiko dhidi yake ni chimbuko la uamuzi wa bunge na kutaka apewe mwongozo wa suala hilo kuendelea kujadiliwa wakati mahakama kuu imeshazuia huku akilitaka baraza hilo kutokuingia kwenye misukumu ya kisiasa badala yake wafuate sheria za nchi na kukabidhi hati hiyo kwa mwenyekiti wa baraza.
Hata hivyo mara baada ya kutoka nje ya ukumbi waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari walipotaka kufanya naye mahojiano juu ya suala hilo Mh Chenge majibu yake yalikuwa hivi.
Mwenyekiti wa baraza hilo jaji mstaafu Hamisi Msumi akizungumza mara baada ya kuahirisha zoezi hilo amesema amelazimika kufanya hivyo ili wapate fursa ya kupitia zuio hilo ili kila upande uweze kupata haki.
Kwa upande wa wanasheria wa sekretarieti ya baraza hilo wamepinga hoja alizotoa mh Chenge na kudai kuwa wao walipitia zuio hilo na kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kumuta na awali walishafanya naye mahojiano lakini hakutoa hoja hizo.
Social Plugin