Licha ya Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) kufuta usajili na kupiga marufuku uuzaji wa dawa duni, zenye madhara na zisizofaa kwa matumizi ya binadamu, dawa hizo zimegundulika kuuzwa holela na baadhi ya wamiliki wa maduka ya dawa katika kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza.
Hayo
yameelezwa na wakazi wa Kisesa wilayani Magu, wakati wa semina ya siku
moja iliyojadili visababishi vya ulemavu katika jamii, ambapo walisema
madhara ya ulemavu yanatokana na watu kutumia dawa zilizopita muda wake.
Semina
hiyo ilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 50 kutoka katika makundi ya
walemavu wa kutoona, viungo, kutosikia, uono hafifu, ngozi na watendaji
wa vijiji na vitongoji, iliyoandaliwa na asasi ya watu wenye ulemavu ya
SANJO na kufadhiliwa na Shirika la the Foundation for Civil Society.
Wananchi
hao waliiomba Serikali kupitia TFDA, kuwachukulia hatua wamiliki hao wa
maduka wanaoendelea kuuza dawa hizo zilizofutiwa usajili kwa madai kuwa
zinaweza kuwasababishia madhara na pengine vifo.
Dawa
zilizofutiwa usajili na TFDA ni dawa ya kutibu fungus (ya vidonge na
kapsuli) aina ya Ketoconazole, dawa za kutibu mafua na kikohozi za maji,
vidonge na kapsuli zenye kiambato hai aina ya phenylpropanol amine na
dawa ya kuua bakteria ya sindano, aina ya Chloramphenicol Sodium
Succinate.
Zingine
ni dawa ya kuua bakteria ya maji na kapsuli aina ya cloxacillin,
malaria ya vidonge yenye mchanganyiko wa Sulphadoxine na
Pyrimethamine(SP) na dawa aina ya Amikacin, Levofloxacin.
Watoa
huduma pia waliagizwa kusimamia mabadiliko ya matumizi ya dawa aina ya
SP ili ziweze kutumika kwa wajawazito tu na dawa aina ya kanamycin,
amikacin na Levofloxacin zitumike kwa wagonjwa wa kifua kikuu tu kwenye
hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Akizungumza
katika semina hiyo, mkazi wa Kisesa, Romanus Kalista alisema licha ya
Serikali kupitia TFDA kubaini kuwepo kwa dawa duni kwa watumiaji na
kufuta usajili wake kwa matumizi ya binadamu, anaona hali hiyo
imewachanganya wananchi kutokana na ukweli wananchi wengi kabla ya
kufutiwa usajili, walikuwa wakizitumia.
“Dawa
hizi hizi zimetumiwa na wananchi kwa muda mrefu, je wananchi waliokuwa
wakizitumia endapo watagundulika kupata madhara nani atawahudumia, na
ukweli ni kuwa kama zilikuwa na madhara wananchi nao watakuwa
wameathirika”, alihoji.
Aliongeza, “Hata
hivyo dawa hizo zilizopigwa marufuku bado zinatumika hapa Kisesa na
TFDA bado haijatoa elimu ya kutosha kwa wananchi, na kibaya ni kwamba
dawa hizi bado zinauzwa kwenye maduka ya dawa.”
Alisema
yeye binafsi anashangaa kusikia serikali imetangaza kufuta usajili wa
baadhi ya dawa zilizoharibika, ambazo vijijini zilikuwa zinatumiwa na
wananchi na kuhoji kuwa kama dawa hizo hazina ubora ni kwanini zisipigwe
marufuku zinakotengenezwa hususan viwandani.
Kwa
upande wake, Agnes Mathias ambaye ni mkazi wa Kisesa na ambaye alikiri
kuwa aliwahi kufanya kazi ya kuuza dawa katika duka la dawa, aliitaka
Serikali itoe elimu zaidi kwa umma.
“Bado
dawa zilizopigwa marufuku zinauzwa huku kwetu, mimi nilikuwa muuzaji
najua mbinu zinazotumika kuuza dawa, wauzaji wanauza kwa kufungua mlango
kidogo, ningeomba serikali ingetuma wataalam waje kufanya ukaguzi
vinginevyo madhara yatakuwa makubwa”, alionya.
Kwa
upande wake, mkazi wa Kisesa John Alphonce licha ya kuitaka Serikali
kupambana na mila potofu juu ya watu wenye ulemavu, alisema kuwa baadhi
ya dawa wanazotumia akinamama wajawazito husababisha ulemavu kwa mtoto
anayezaliwa.
“Na
kwa sababu hiyo mimi sikubaliani na hoja kuwa ulemavu ni mpango wa
Mungu, inawezekana mama anaweza akawa amemeza dawa au kuchomwa sindano
wakati wa ujauzito na baadae mtoto anayezaliwa hupata ulemavu”, alisema.
Mwezeshaji
wa semina hiyo, Mwanasheria wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Mwanza
(CHAWATA), Revocatus Almasi aliitaka jamii kushiriki kamilifu katika
kukabiliana na changamoto zinazowapata watu wenye ulemavu nchini na
waachane na mila potofu.
“Kutokana
na mila zilizopitwa na wakati, jamii inaamini kuwa watu wenye ulemavu
ni tegemezi, wasio na uwezo,wanastahili kusaidiwa na watu wasio na
ulemavu ili waweze kumudu maisha yao”, alisema.
Mkurugenzi
wa SANJO, Joseph Msuka alisema lengo la semina hiyo ilikuwa ni
kuelimisha jamii kupitia kwa watu wenye ulemavu na watendaji wa vijiji
na kata wajue madhara yakuteketeza watoto wanaozaliwa na ulemavu
kunakofanywa na baadhi ya watu katika jamii, hasa wanaume na baadhi ya
akinamama kutumia dawa zilizopita muda wake wa matumizi.
Akizungumza
na Mpekuzi kwa njia ya simu kutoka mkoani Iringa, Kaimu Meneja wa TFDA
Kanda ya Ziwa, Moses Mbamba alisema wamiliki wa dawa wanaouza dawa hizo
zilizofutiwa usajili, wanajali zaidi kutafuta pesa kwa gharama ya maisha
ya watu kuliko kujali uhai wa binadamu. Alisema ofisi yake itafanya
ukaguzi wa haraka katika eneo hilo.
“Kesho
nitamuagiza msaidizi wangu aende huko mara moja kufanya ukaguzi na
watakaobainika tutawafikisha mahakamani mara moja, hatutakubali wao
kuendelea kuuza dawa zilizofutiwa usajili,” aliahidi.