Wakati
mbio za urais zikiendelea kukolea,mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za
Mitaa (ALAT) mkoa wa Shinyanga Justine Sheka(Pichani) amewataka viongozi kutoka
kanda ya ziwa waliotangaza nia ya kugombea urais waunganishe nguvu kwa Edward
Lowassa huku akimtaka Lowassa kuchukua fomu mapema kwani historia inaonesha
kuwa ndiyo kiongozi pekee wa kuitawala Tanzania katika kipindi hiki.
Sheka
aliyasema hayo juzi mjini Shinyanga wakati akizungumza na waandishi wa habari
ambapo alisema Jumuiya ya serikali za mitaa mkoa wa Shinyanga inaamini kuwa
Lowassa ndiye kiongozi atakayeweza kuivusha nchi ya Tanzania hapo ilipofikia.
Sheka
ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,alisema watu
wanaoendelea kumuwekea pingamizi Lowassa hawaitakii mema nchi kwani historia
inaonesha kuwa watanzania wengi bado wanamwitaji hasa wakikumbuka kazi nzuri
aliyoifanya yeye binafsi wakati akiwa waziri mkuu kwa muda mfupi ,katika
harakati za ujenzi wa shule za sekondari za kata ambazo hadi sasa zipo.
“Mimi kwa
kushirikiana na wenyeviti wote wa ALAT wa halmashauri zote za wilaya pamoja na
wajumbe walioko katika wilaya wa mkutano mkuu wa taifa wa Chama Chama
Mapinduzi,tunamtaka Lowassa akachukue fomu mapema na asiwekewe kipingamizi cha
aina yoyote”,alieleza Sheka.
“Tunaomba
katika kanda ya Ziwa Victoria wagombea wengine wamuunge mkono mzee Lowassa kwa
sababu tunaona nafasi ya urais inamfaa na kimsingi ndiyo chaguo la watu
wengi na historia inaonesha kuwa anafaa kuiongoza Tanzania”,aliongeza Sheka.
Alisema ni
vyema waliotangaza nia ya kugombea nafasi hiyo nyeti ya urais kuunganisha nguvu
kwa Lowassa ili wakati wa kuunda serikali wapatikane viongozi wazuri wa
kuingoza nchi ambayo sasa inapitia katika changamoto mbalimbali.
“Kuhusu
John Magufuli kushawishiwa kuchukua fomu ya kugombea urais ni jambo jema
,tunaamini ni kiongozi mchapa kazi sana,kwa mawazo yetu tunadhani ni bora
angeunganisha kwa Lowassa ili itakapofikia wakati wa kuunda serikali basi
wamwangalizie nafasi ya uwaziri mkuu ili kufanya kazi za serikali ziendelee
vizuri kwa jopo litakuwa zuri sana”,alieleza Sheka.
Na Kadama Malunde-Shinyanga