Kijana
mmoja, Omary Ramadhani, 28, (pichani) mkazi wa Sinza Madukani, Dar
amenusurika kifo baada ya kupata ajali ya kugongwa na ‘Break Down’
alipokuwa akiendesha Bajaj katika makutano ya Barabara ya Sam Nujoma na
Ali Hassan Mwinyi, Mwenge, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa
masikitiko, Omary alisema kuwa alipogongwa na gari hilo hakuweza
kujitambua kwani hata wasamaria wema walivyomchukua na kumkimbiza
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, walijua alifariki dunia hivyo
wakamuingiza moja kwa moja mochwari, lakini kwa bahati nzuri alitokea
nesi mmoja aliyeshauri asiwekwe kwanza kwenye friji mpaka apimwe.
Akiendelea kuzungumza kwa
tabu kutokana na maumivu ambayo anayo, Omary alisema baada ya nesi huyo
kumpima aligundua alikuwa akipumua kwa shida.
Alisema hata ndugu zake
walijua ameshafariki dunia kutokana na alivyokuwa, kwani alivunjika
mgongo mara sita na mfupa wa mkono ulitoka nje na kupasuka kichwani
jambo lililosababisha kuvuja damu nyingi.
Alifafanua kuwa kutokana
na hali yake, alikimbizwa katika chumba cha wagonjwa mahututi ambapo
baada ya siku tatu alizinduka na walipokuja ndugu zake aliwauliza
alikuwa wapi, walipomuambia Muhimbili alizimia tena.
Alisema alipata matibabu
kwa muda wa miezi sita ndipo aliruhusiwa kuondoka lakini alitakiwa atoe
shilingi 1,000,000 kwa ajili ya tiba maalum kwenye mashine ambayo
siijui jina, lakini nimeshindwa kuzipata na ndugu zangu ni walalahoi.
Omary alisema hivi sasa
bado ana matatizo, haja ndogo haitoki sawasawa na akienda maliwatoni
huchukua zaidi ya saa moja kwani mkojo hutoka kidogokidogo na
kumsababishia maumivu makali ambapo haja kubwa anapata mara moja kwa
wiki.
Omary amewaomba
Watanzania wenye moyo wa huruma kumchangia ili atibiwe, aepukane na
mateso makali anayopata. Namba yake ni 0656 168 034.