Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Tanga,
kimevunjika mara tatu mfululizo kutokana na madiwani wa Chama cha
Wananchi (CUF) na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanyiana vurugu na
kukunjana kutaka kuzichapa kavu kavu.
Vurugu hizo zimetokana na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga
kuendelea kumtambua na kumwita katika vikao vya Baraza la Madiwani wa
jiji hilo aliyekuwa Diwani wa Kata ya Malungu (CUF), Mohamed Mwambeya,
wakati alishajiondoa katika chama hicho.
Mwambeya ambaye alipata udiwani wa kata hiyo kupitia CUF, Agosti,
mwaka jana, alitangaza kukihama chama hicho na kuhamia CCM wakati wa
mkutano wa Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Abdallah
Bulembo alipofanya ziara mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, nafasi zote
za kuchaguliwa za kisiasa kwa maana ya rais, ubunge na diwani, ni lazima
atokane na chama cha siasa na masharti hayo pia yapo katika uchaguzi wa
serikali za mitaa.
Hivyo kutokana na katiba hiyo, Mwambeya ambaye alitangaza kujiondoa
CUF na kujiunga CCM ni wazi kuwa udiwani wake utakuwa umekoma na
msimamizi wa uchaguzi alistahili kutangaza kuwa kata hiyo ipo wazi ili
kufanyike mchakato wa kuchagua diwani mwingine atakayetokana na chama
cha siasa.
Wakati wa kikao cha jana, vurugu zilizuka baada ya madiwani wa CUF
kupinga Mwambeya kuhudhuria kikao hicho hali iliyosababisha polisi
kuingilia kati na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha Jeshi
la Polisi Mkoa wa Tanga kutuliza vurugu kisha kikao kuahirishwa.
Vurugu hizo zilianza saa 3:00 asubuhi baada ya Meya wa Jiji hilo, Omar Gulled, kufungua kikao hicho.
Baada ya Meya Gulled kuingia kwenye ukumbi wa jiji hilo, madiwani
hao walisimama na kupiga makofi na hata baada ya kuketi madiwani wa CUF
waliendelea kugonga meza mfululizo, hivyo kikao kushindwa kuendelea na
kuahirishwa kwa nusu saa.
Baadaye madiwani waliingia tena ukumbini kwa lengo la kuendelea na
kikao hicho badala yake yalianza malumbano ya kutupiana maneno ambayo
nusura madiwani wa CUF na CCM wazichape.
Wakati hali hiyo ikiendelea, Diwani Mwambeya anayetuhumiwa
kuendelea kuhudhuria vikao hivyo kupitia CUF, alinyanyuka kwenye kiti
chake na kwenda kumpora gazeti Diwani wa Viti Maalum wa CUF na kulichana
hali iliyosababisha kuzuka zaidi kwa vurugu kwenye ukumbi huo.
Licha ya Meya Gulled kuingia kwa mara ya pili kuendesha kikao cha
baraza hilo, aligonga mwamba kwa sababu hakukuwa na maelewano kutokana
na madiwani hao kuendelea kugonga meza na kusababisha kuvunjika kwa
mara ya pili.
Vurugu hizo zimesababisha halmashauri hiyo kushindwa kuendesha
vikao saba kama hivyo tangu kutokea kwa tukio hilo kama hilo la Mwambeya
kujiondoa CUF lakini wakati huo akiendelea kuitwa katika vikao vya
Baraza la Madiwani.
Akizungumza baada ya kuvunjika kwa kikao hicho, Diwani wa Kata ya
Ngamiani Kusini (CUF), Mussa Mbaruku, alisema wamefanya vurugu hizo ili
kupinga halmashauri hiyo kuendelea kumtambua Diwani wa Kata ya
Marungu, Mohamed Mwambeya kama mwakilishi wa kata hiyo kwa chama hicho
wakati alikihama na kujiunga na CCM tangu mwaka jana.
Mbaruku ambaye pia ni Mwenyekiti wa Madiwani wa CUF alisema
Mwambeya alitangaza kujiunga na CCM kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika Tangamano ambao ulihutubiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi ya CCM Taifa, Bulembo.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi) ibara ya 21 (1-2), sababu za diwani kupoteza nafasi
yake ikiwamo kuhama chama kilichompa uongozi.
“Ibara ya 41 (1) ya sheria hiyo inataka apewe barua na Ibara ya 41
(2) Waziri wenye dhamana anatakiwa kutangaza nafasi hiyo kuwa wazi baada
ya siku 90... sasa ni zaidi ya miezi sita kuna nini hapa?” Alihoji
Mbaruku.
Alidai vurugu wanazozifanya ni moja ya njia ya kufikisha ujumbe
kwa halmashauri hiyo na kwa Waziri mwenye dhamana kwa kupitia kikao
hicho badala ya kuandamana barabarani.
Madiwani hao walimtupia lawama Meya wa Jiji hilo wakidai anatumika
kutekeleza matakwa ya CCM na kwamba amekuwa mzigo kuleta maendeleo ya
wakazi wa jiji hilo kutokana na kutofanyika kwa vikao vya baraza hilo.
Vilevile walilaani kitendo cha kuitiwa polisi wakisema ni ushahidi
wa kukisaidia CCM kwani kanuni haziwaruhusu askari hao kuingilia
shughuli za mabaraza hayo na hatua hiyo ni ya kuwatisha.
Meya Gulled alipohojiwa na NIPASHE kuhusiana na tukio hilo,
alielezea kusikitishwa na kuwataka madiwani hao kufuata kanuni,
taratibu na sheria badala ya kufanya vurugu.
Alisema baada ya tukio la diwani huyo, kwa nafasi yake amewajibika
kwa kumuandikia barua Waziri wa Tamisemi kwenye dhamana kwa sababu siyo
wajibu wake wa kuchukua hatua dhidi yake.
Meya huyo alisema athari za vurugu hizo ni pamoja na kutofanyika
vikao vya baraza ambavyo ndiyo dira na mwongozo wa halmashauri hiyo
kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kwa upande wake Mwambeya akizungumzia vurugu hizo, aliponda madai
hayo huku akisisitiza kuwa kuwa yeye ni diwani na mwana-CUF safi, hivyo
hayo ni majungu na uoga wa kimadaraka kwa viongozi wa chama hicho.
Alisema hajaitwa na chama chake kuhusiana na tukio hilo na kama ni
barua alijibu kueleza kuwa licha ya kujitangaza na kuchukua kadi ya CCM
lakini bado ni mwana-CUF kutokana na ukweli kuwa hajairejesha kadi yake
popote.
Wakati wa mkutano wa Bunge la 16 na 17, Mbunge wa Viti Maalum CUF,
Magdalena Sakaya, alimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu sakata
la diwani Mwambeya na kuahidi kuwa atalishughulikia.
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, alipotafutwa azungumzie suala
hilo, licha ya kupigiwa simu yake mara kadhaa, ilikuwa ikiita bila
kupokelewa.
Na Dege Masoli-Nipashe
Social Plugin