Tukio la kurushiana risasi kati ya polisi wakishirikiana na
askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya watu
wanaosadikiwa kuwa majambazi au magaidi limeacha maswali 10 muhimu
yanayolifanya lionekane lenye utata.
Mpaka sasa hakuna taarifa za kina juu ya tukio
hilo lililotokea siku nne zilizopita na kusababisha kifo cha mwanajeshi
na wapiganaji wengine zaidi ya sita ambao hawajajulikana kujeruhiwa.
Jana katika mkutano wake na waandishi wa habari
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Magalula Said Magalula alijaribu kujibu baadhi
ya maswali hayo ambayo yamewafanya wananchi wa Tanga na mikoa mingine
nchini, kupata taharuki na kufananisha tukio hilo na matukio ya kigaidi
yanayotokea katika nchi mbalimbali duniani.
Hata hivyo, majibu ya Magalula, kama ilivyokuwa
katika taarifa ya awali iliyotolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo
wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, yaliwaacha waandishi wa habari na
maswali mengi kuliko majibu, kwani mbali na kuwatoa hofu wananchi, kuna
maswali aliyajibu kwa kifupi bila ufafanuzi wa kutosha, hivyo kuzidi
kulifanya tukio hilo kuwa na utata.
Swali la kwanza ambalo wananchi wanajiuliza ni iwapo tukio hilo ni la kigaidi au ujambazi?
Akijibu swali hilo na kukataa kuulizwa swali la aina hiyo tena, Magalula alisema tukio hilo ni la ujambazi.
Kauli ya mkuu huyo wa mkoa inafanana na ya Waziri
wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mathias Chikawe ambaye juzi aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa tukio hilo ni la uhalifu wa kawaida.
Alisema polisi wanafahamu kuwa kuna hali ya hatari
na wameshaongeza ulinzi katika maeneo yote, kwamba juhudi zaidi
zinaendelea kufanyika ili kulinda usalama wa raia na kuifanya Tanzania
ibaki kuwa kisiwa cha amani.
Swali la pili, waliohusika katika mashambulizi hayo ni raia wa nchi gani?
Magalula alisema swali hilo halina majibu na
kwamba majibu yake yatapatikana baada ya kukamatwa kwa watu hao
wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Juzi, Kamishna Chagonja alikaririwa akisema
mapigano hayo yalifanyika katika msako wa majambazi walioiba silaha
kwenye kituo cha polisi mkoani Tanga, huku taarifa nyingine zikisema
mmoja wa watuhumiwa tayari alikuwa mikononi mwa polisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi
Makosa ya Jinai nchini (DCI), Diwani Athumani alisema matukio ya uhalifu
yanayotokea nchini ni mapya na yanayochochewa na ukuaji wa teknolojia
ya habari na mawasiliano.
Swali la tatu ni iwapo wahalifu hao waliuawa katika mashambulizi au walitoroka na walipita wapi?
Katika majibu yake Magalula alisema hakuna mwili wowote ulioonekana au kuokotwa na operesheni ya kuwasaka bado inaendelea.
Swali la nne, ni juu ya eneo la Amboni
yalipotokea mashambulizi kama lina mapango yanayoishia mkoani humo au
yanatokezea hadi nchi jirani kama inavyodaiwa?
Pamoja na Magalula kusema kuwa kuna simulizi
nyingi ambazo hazina uhakika juu ya pango hilo, mkazi mmoja wa eneo hilo
ambaye hufanya kazi ya kupiga picha alisema eneo la Amboni lina jumla
ya mapango 13 yaliyogunduliwa lakini yanayotumika ni mawili. Mapambano
yamefanyika katika pango la mbali na lile linalotembelewa na wageni.
Swali la tano, ni juu ya waliojeruhiwa katika tukio hilo?
Magalula alisema waliojeruhiwa ni askari wa JWTZ
na polisi na wamelazwa katika hospitali ya Bombo, lakini hadi sasa
hawajatajwa majina.
Mbali na maswali hayo, pia wananchi wanajiuliza
maswali mengine ambayo ama hayajapata majibu au majibu yake
hayajawaridhisha, kama vile, Je, lengo la uvamizi lilikuwa nini,
mtuhumiwa aliyekuwa anashikiliwa na polisi alitorokaje, je, alikuwa
amefungwa pingu na iwapo sasa kuna uhakika wa usalama?
Maelezo ya ziada
Akitoa maelezo zaidi juu ya tukio hilo, RC
Magalula alisema hadi jana mchana hakukuwa na mtu yeyote aliyekamatwa
kuhusiana na tukio hilo.
Alisema kufuatia hali hiyo, maofisa wa vikosi vya
ulinzi na usalama wameahamia kwenye mapango mengine ili kujiridhisha
kama wahalifu hao watakuwa wamejificha huko.
“Kama inavyofahamika eneo la Amboni lina mapango
zaidi ya 13, hili lililofanyiwa mashambulizi liko umbali wa kilomita
tano kutoka lile linalotumika kwa utalii, kwa hiyo ili kujiridhisha ni
lazima maofisa wakague sehemu zote,” alisema Magalula.
Mkuu huyo wa mkoa alisema hali sasa imerejea kuwa shwari na amewataka wananchi kuendelea na shughuli zao.
Alipotakiwa na waandishi wa habari kufafanua kwanini aseme hali
ni shwari wakati hakuna hata jambazi aliyekamatwa wala silaha
zilizotumika kuwashambulia askari akiwamo Sajenti Said Kajembe
aliyeuawa, Magalula alijibu kwa kifupi kuwa ni kwa sababu vyombo vya
ulinzi na usalama vimeshatafuta kila pembe ya Tanga na kujiridhisha.
“Serikali ina mkono mrefu imeshatafuta kila pembe
ya Tanga na imejiridhisha kwamba hali ni shwari na ndiyo maana nipo hapa
kuwaeleza wananchi waendelee na kazi zao,” alisema Magalula.
Eneo la utalii
Kuhusu eneo la utalii la mapango ya Amboni,
Magalula alisema halikuguswa wala wahalifu hawakuwa wamejificha huko na
ndiyo maana shughuli za kuwapokea na kuwatembeza wageni zilikuwa
zikiendelea.
Mwananchi ilikwenda katika lango kuu la mapango ya
utalii ya Amboni ambako mhifadhi mkuu, Jumanne Gekora alisema tukio la
mashambulizi limeathiri shughuli za mapango hayo.
Mhifadhi huyo aliviomba vyombo vya habari
viifahamishe jamii kwamba sehemu iliyoshambuliwa si hapo kwenye utalii
bali ni umbali wa zaidi ya kilomita tano na ni mapango ambayo hayapo
hata kwenye utaratibu wa kuwatembeza wageni.
Hospitalini Bombo
Habari kutoka hospitalini walikolazwa majeruhi
watano ilielezwa kuwa hali zao zinaendelea vizuri ingawaje bado
waandishi wa habari hawajaruhusiwa kwenda kuwaona na hawakutajiwa majina
yao.
Wakati huohuo askari aliyeuawa katika mashambulizi
hayo,Sajent Said Kajembe (47) wa kikosi cha 37 JWTZ amezikwa leo katika
kijiji cha Bungu kata ya Dindira Wilayani Korogwe akiwa ameacha mjane
na watoto watatu.
Mdogo wa marehemu, Bakari Kajembe alisema familia
yao imepokea kwa masikitiko kifo hicho kwa sababu Sajenti Said alikuwa
tegemeo kwao kutokana baba yao kufariki dunia miaka ya nyuma.
Na Burhani Yakub, Mwananchi
Na Burhani Yakub, Mwananchi
Social Plugin