Mwanamke mmoja amefariki dunia mkoani Iringa baada ya kutokea kwa vurugu kati ya askari polisi na wananchi maeneo ya Ilula wilaya ya Kilolo ambapo jeshi la polisi pia linawashikilia wananchi 18 wa eneo hilo kwa mahojiano zaidi.
Hayo
yamesemwa leo na kaimu Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa ACP
Pudensiana Protas wakati akiongea na waandishi wa
habari ambapo amemtaja aliyefariki katika vurugu kuwa ni bi Mwaine Mtandi (25) mkazi wa
kijiji cha Dingizayo wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.
Amesema mwanamke huyo alikuwa akijihusisha na uuzaji
wa pombe za kienyeji na alifariki papo hapo baada ya kuanguka wakati
akijaribu kuwakimbia polisi waliokuwa kwenye oparesheni ya kukamata
makosa mbalimbali ya jinai.
Kaimu
Kamanda Protas amesema tukio hilo limetokea jana majira ya
saa nne na nusu asubuhi wakati polisi wakiwa kwenye zoezi la kawaida la
msako wa makosa mbalimbali ya jinai ikiwa ni pamoja na kuwakamata
wanaojihusisha na vitendo vya uuzaji wa pombe haramu ya gongo na
ufunguaji wa vilabu vya pombe za kienyeji muda wa kazi.
Amesema
baada ya kutokea kwa kifo hicho wakazi wa eneo la Ilula walianza
kuandamana kisha kuifunga kwa kuichoma moto barabara kuu ya Iringa-Dar
es Salaam ,wakitumia tairi za magari,nyasi na karatasi hali iliyopelekea
kusimama kwa shughuli za usafirishaji kwa magari kutoka mikoa ya
Morogoro na Dar es Salaam pamoja na Mbeya,Njombe na Ludewa.
Aidha
amesema wananchi hao walivamia kituo kidogo cha polisi cha Ilula na
kuvunja vioo vitano,kuchoma moto nyaraka mbalimbali pamoja na kuteketeza
kwa moto magari matatu ambayo ni gari la kituo hicho,gari la mmoja wa
polisi wa kituo hicho pamoja na gari moja ambalo lilikuwa limekamatwa
kama kielelezo.
Kaimu
Kamanda Protas ameongeza kuwa wananchi hao walitumia silaha mbalimbali
za jadi ikiwa ni pamoja na mawe,rungu na mapanga hali iliyopelekea
majeruhi kwa askari watano ambapo wanne walipata huduma ya kwanza na
kuruhusiwa na mmoja wao bado anaendelea na matibu katika hospitali ya
mkoa wa Iringa.
Amesema kufuatia vurugu hizo jeshi la polisi mkoani Iringa
linawashikilia watu 18 kwa uchunguzi zaidi huku wananchi wawili
wakiendelea na kupatiwa matibabu katika hospitali teule ya wilaya ya Kilolo baada ya kujeruhiwa katika vurugu hizo.
Kaimu
kamanda Protas ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Iringa kwa ujumla
kutojichukulia sheria mkononi pindi yanapotokea matukio mbalimbali na kuongeza kuwa uchunguzi zaidi wa vurugu hizo unaendelea ikiwa ni
pamoja na kubaini chanzo halisi cha mauaji hayo.
Hali
hiyo imekuja kutokana kutofautiana kwa wakzi wa eneo hilo juu ya chanzo
cha halisi cha mauaji hayo ambapo wapo waliodai kifo hicho kimetokana
na marehemu kupigwa risasi,na wengine kuongeza kuwa alipigwa rungu huku
baadhi yao wakidai kuwa alipigwa mtama na polisi katika harakati za
kumkamata marehemu.
Na Yonna Mgaya-Malunde1 blog Iringa
BOFYA MANENO HAYA KUANGALIA PICHA KATIKA VURUGU HIZO ZA POLISI NA WANANCHI
BOFYA MANENO HAYA KUANGALIA PICHA KATIKA VURUGU HIZO ZA POLISI NA WANANCHI
Social Plugin