Kibano! Jamaa mmoja ambaye jina halikupatikana mara moja, amejikuta
akinusa kifo baada ya kula kipigo ‘hevi’ wakati akifanya jaribio la wizi
wa fedha kiasi cha shilingi laki 450,000 kupitia huduma za fedha kwa
mitandao ya simu.
Tukio hilo lilmtokea mwishoni mwa wiki
iliyopita maeneo ya Kijitonyama jijini Dar es salaam ambapo jamaa huyo alidaiwa
kuingia kwenye duka moja akijifanya anataka kutoa shilingi laki nne na
nusu (450,000/=) jambo lililomfanya wakala kumuonesha namba za kutolea
kwa uchangamfu akijua ni mteja wa kawaida.
Dakika chache baadaye wakati wateja wengine wakiendelea kuhudumiwa,
jamaa huyo alionesha meseji kuwa ametoa kiasi hicho cha fedha kupitia
moja ya mitandao ya simu.
Wakala huyo alipoichukua meseji ya jamaa huyo ili kuhakikisha muamala
wake alishangaa kuona meseji hiyo kuwa ni ya mtandao mwingine tofauti na
alioutaja huku ikionesha imeandikwa au kutumwa na namba ya kawaida ya
simu badala ya namba ya huduma hiyo ya mtandao husika.
Wakizidi kumshushia kichapo.
Wakala huyo, Maulid Vedasto alishangaa na kuamua kumshikilia jamaa huyo
akimuitia mwizi ndipo wananchi wenye hasira kali walipofika na
kumzingira wakimtaka atoe maelezo ya kutosha ambapo njemba huyo ilikiri
kutaka kuiba jambo lililoamsha hasira za watu walioamua kumshushia
kipigo hevi nusura afe.
Wakala huyo alisema kuwa jamaa huyo alifika mara ya
kwanza siku hiyo dukani kwake akitaka kutoa shilingi elfu sabini lakini
alighairi na kurudi baada ya muda mfupi akitaka kufanya jaribio hilo la
wizi.
Kichapo kikiendelea.
“Nilianza kumtilia shaka mara ya kwanza alipokuja na kujifanya anataka
kutoa fedha huku akiwa na wasiwasi na kila mara alipokuwa akiwaona watu
wengi ndipo alipokuwa akiniongelesha akijifanya ana haraka ya kutoa
fedha, akiona watu wachache anasubiri,” alisema wakala huyo.
Baada ya
kunaswa jamaa huyo alipekuliwa kwenye simu yake ambapo iligundulika kuwa
kweli meseji hiyo haikuwa ya mtandao husika huku akiwa hana salio.
Katika kuhakikisha hilo, wakala huyo aliwapigia simu makao makuu ya
mtandao huo na kupata taarifa kuwa hakuna salio la aina hiyo
lililohamishwa kutoka kwenye simu ya jamaa huyo.
Katika utetezi wake,
jamaa huyo aliomba watu wasimuue kwa kuwa ni tamaa za kidunia zilimponza
huku akikiri kufanya utapeli huo kwa kushirikiana na wenzake watatu
ambapo wamefanikiwa kutapeli mawakala kibao jijini Dar es salaam.
“Jamani
inatosha mlivyonipiga, naomba msiniue ni shetani tu amenipitia. Kweli
nakiri kuwa nimewaibia mawakala wengi sana lakini nimekoma. Nipelekeni
polisi msiniue,” alisema jamaa huyo ambaye alikuwa akivuja damu
chapachapa kisha kupelekwa Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’
kusubiri sheria kuchukua mkondo wake.