KUHUSU BINTI ALIYEMUUZA MAMA YAKE MAITI ITUMIKE KWA TAMBIKO ILI APATE SHILINGI MILIONI 10

JESHI la polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Sophia Chambo(30)mkazi wa mtaa wa eneo la polisi kata ya Lizaboni mjini Songea kwa tuhuma ya kumuuza mama yake mdogo kwa mfanyabiashara mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa anaedaiwa kuwa alishawishiwa apate zindiko la biashara yake ili afanikiwe kwa kuuziwa maiti ambayo aliahidiwa kuuziwa kwa shilingi milioni kumi.

Habari zilizopatikana jana mjini Songea na kuthibitishwa na kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Mihayo Msikhela zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Februari 17 mwaka huu majira ya saa nane mchana katika eneo la Lizaboni mjini Songea ambako Anitha Kasimu Mbawala(40)mkazi wa kata ya Ruvuma mjini Songea yalifanyika mazungumzo ya kutaka kumuuza kwa mfanyabiashara huyo.

Akifafanua zaidi kamanda wa polisi kuwa inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio Sophia alimfuata mtu mmoja ambaye jina lake linaendelea kuhifadhiwa kwa sababu za kiusalama na kumuambia kuwa ili aweze kufanikiwa katika biashara zake inabidi afanye zindiko kwa kutumia maiti ya binadamu.

Alieleza zaidi kuwa Sophia alimuambia mtu huyo kuwa kwa sasa wafanye biashara kati yake na mfanyabiashara huyo  kwa sababu yeye ana mama yake mdogo aliyemtaja kuwa ni Anitha ambaye alikuwa na ugomvi nae hivyo ampatie kiasi cha shilingi milioni kumi ili akamuuwe na amletee maiti ya mama huyo ikiwa imehifadhiwa kwenye gunia.

Kamanda Msikhela aliendelea kufafanua kuwa inadaiwa mfanyabiashara huyo alikataa kuletewa maiti na badala yake alimueleza Sophia kuwa aletewe mtu mzima au akiwa hai na akamuambia kuwa atamuua yeye mwenyewe ila Sophia amlete mama yake mdogo akiwa mzima na kuwa alimuomba Sophia ampunguzie bei badala ya shilingi milioni kumi amuuzie kwa shilingi milioni 6.5.

Alisema kuwa baada ya kukubaliana mfanyabiashara huyo alitoaq taarifa kwa jeshi la polisi juu ya tukio hilo na askari polisi wakiwemo askari kanzu kutoka ofisi ya Afisa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Ruvuma ambao waliweka mtego wa kuhakikisha kuwa wanamnasa Sophia.

Alisema kuwa Februari  18 mwaka huu majira ya asubuhi Sophia alikwenda Ruvuma kumfuata mama yake mdogo kwa kumdanganya kuwa kuna mwanaume amempenda mama yake alikataa ndipo Sophia alipomrubuni tena na kumueleza kuwa kuna matajiri wanataka mtu wa kumuajiri ndipo Anitha alipokubali na kupelekwa mpaka Lizaboni katika eneo walilokuwa wamepanga kukutana mnunuzi waliekubaliana siku ya nyuma yake.

Alisema kuwa inadaiwa kuwa ilipofika majira ya saa 5;30 katika eneo hilo la Lizaboni askari polisi walifanikiwa kumkamata Sophia akiwa na mama yake mdogo tayari kwa kumuuza na kabla yake mfanyabiashara huyo alikuwa amekwenda benki kuchukua fedha kwa ajili ya kumlipa Sophia ndipo polisi walipomkamata.

Hata hivyo kamanda Msikhela alisema upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili. 
Na Gideon Mwakanosya- Songea

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post