Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATU WANAODAIWA KUWA MAGAIDI WAUA ASKARI WA JWTZ NA KUJERUHI POLISI HUKO TANGA

 
Askari mmoja wa jeshi la wananchi ameuawa kwa kupigwa risasi huku wengine wanne wa jeshi la polisi wamejeruhiwa vibaya na kulazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo kufuatia mashambulizi ya kurushiana risasi katika mapango kati yao na vikundi vinavyodaiwa kuwa vya kigaidi.



Habari kutoka katika eneo la tukio zinadai kuwa vikundi hivyo vilikuwa ndani ya mapango huku askari wakiwa nje hatua ambayo imedaiwa kuwa majibizano ya risasi yalisababisha askari wa jeshi kupigwa ya tumboni na kuwahishwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo lakini baadae alifariki dunia.

 Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo CP Paul Chagonja aliyelazimika kusafiri kwa helkopta kutoka Dar es salaam kwenda Tanga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema kuwa si tukio kubwa kama linavyoelezwa na baadhi ya watu na kwamba waliohusika ni majambazi na siyo magaidi.

 Changonja akielezea tukio hilo amekiri kuwa askari wake watatu na mmoja wa jeshi la wananchi wamejeruhiwa kwa risasi wakati askari wake walipoingia katika mapango hayo ndipo mmoja kati ya wanakikundi hao aliporusha risasi na kuwajeruhi askari.

Amesema kilichotokea ni oparesheni ya kawaida iliyofanywa na jeshi la polisi kuwasaka watu wanaosadikiwa kuwa majambazi waliodaiwa kujificha katika mapango hayo na ndipo yalipotokea mapigano hayo yaliyoambatana na kurushiana risasi na kupelekea askari hao kujeruhiwa.

Amesema baada ya hali kuwa tete, jeshi hilo lililazimu kuomba msaada kutoka kwa askari wa jeshi la wananchi Tanzania JWTZ ambao walifika katika eneo la tukio na kufanikiwa kutuliza hali ya taharuki iliyokuwa imetanda katika eneo hilo.

Kamishna Chagonja amesema askari waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo, na kwamba jeshi hilo linaendelea na msako ambapo hadi sasa hakuna alikamatwa.


Alipoulizwa kuhusiana na madai ya kuwepo kwa kifo cha mwanajeshi mmoja,Kamishna Paul Chagonja amesema kuwa Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kutoa taarifa inayohusu wanajeshi wa JWTZ, na kuwataka wanahabari waulizie suala hilo kwa msemaji wa JWTZ.

EATV imemtafuta msemaji wa JWTZ Meja Joseph Masanja ambaye amesema kuwa si jukumu lake kutoa taarifa yoyote kuhusiana na tukio hilo, kwa kuwa tukio hilo ni la kipolisi na siyo la kijeshi.

“Ukitaka kujua taarifa yoyote kuhusu tukio hilo waulize polisi, kwa kuwa hilo ni tukio la kipolisi, sisi huku hatuna taarifa yoyote” amesema Meja Masanja.

Mwanahabari wetu alipotaka kupata taarifa zaidi kutoka katika hospitali ya Bombo ameambiwa kuwa polisi imewazuia kutoa taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo.

Alipojaribu kumuuliza Mkuu wa Mkoa wa Tanga Said Magalula kuhusu kifo cha mwanajeshi mmoja, Mkuu huyo wa mkoa alikiri kupata taarifa za kifo hicho bila kueleza zaidi.
 
Hata hivyo jitihada za waandishi wa habari kwenda katika eneo la tukio ziligonga mwamba baada ya askari polisi wa kikundi cha (FFU) kuweka ulinzi na kudai kuwa hatakiwi mwandishi wa habari kwenda katika eneo hilo huku mganga mkuu wa mkoa wa Tanga Dr,Asha Mahita naye akitoa maelezo kama hayo kuwa waandishi wazuiwe wasiingie katika wodi ya Galanosi kwa ajili ya kuwaona askari waliojeruhiwa.


Kwa mujibu wa mashuhuda ambao ni watu wanaoishi maeneo ya jirani na mapigano hayo pamoja na mwanahabari wetu, wamesema kuwa mapigano hayo yaliyoanza jana usiku na kuendelea hadi usiku kucha na kwamba mwanajeshi mmoja wa JWTZ anahofiwa kuuawa na mwili wake umepelekwa katika hospitali hiyo ya Bombo.

 Baadhi ya wananchi waliozungumza na wanahabari wetu wamesema wameingiwa na hofu kufuatia tukio hilo huku baadhi yao wakidai kuwa wanashindwa kutoka katika nyumba zao kwa kuhofia usalama wao kufuatia milio ya risasi katika eneo la Amboni hasa nyakati za usiku .

CHANZO ITV NA EATV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com