Maajabu!! ALIYEKATIKA MIKONO KWENYE AJALI YA TRENI AWEKEWA MIKONO YA MTU ALIYEFARIKI KWENYE AJALI YA GARI


Madaktari katika Chuo cha Tiba cha Amrita, Kochi huko India wamefanikiwa kufanya upasuaji wa aina yake wa kupandikiza mikono mipya kwa binadamu aliyekatika viungo hivyo. 


Upandikizaji huo uliofanyika Januari 12 na 13, ulifanikiwa kwa mara ya kwanza, baada mwanamume mwenye umri wa miaka 30, aliyekatika mikono katika ajali ya treni kuwekewa mingine. 

Mikono hiyo mipya ilichukuliwa kutoka kwa kijana wa miaka 24 aliyepata aliyefariki katika ajali ya gari.

Mkuu wa kitengo cha upasuaji katika chuo hicho, Profesa Subramania Iyer alisema: “Siku 14 baada ya upasuaji, mikono ilikubaliwa na mwili na ikaanza kujongea, yaani aliyepandikizwa aliweza kuisogeza huku na kule. Mgonjwa alitolewa chumba cha wagonjwa mahututi na huduma nyingine za kumchunguza ziliendelea.”

Daktari katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Muhimbili (Moi), Profesa John Kahamba alisema hiyo si mara ya kwanza kwa upandikizaji wa mikono kufanyika duniani kwani na tofauti kubwa na upandikizaji wa figo au ini.

Jinsi unavyofanyika
Profesa Kahamba alisema upasuaji huo unafanyika kwa kuhakiki mambo mbalimbali ikiwamo uwiano wa kundi la damu, uhai wa seli na misuli na mishipa midogo ya fahamu.

“Upasuaji mkubwa hufanyika, pamoja na kuangalia uwiano wa damu lakini lazima jopo la madaktari wenye kazi tofauti lifanye kazi kwa pamoja. Kwa mfano, wanaounganisha misuli na mishipa midogomidogo na hata wale wa kuhakiki uhai wa seli,” alisema.

Profesa Kahamba alisema kama upandikizaji wa figo unavyofanyika, kadhalika upandikizaji wa mikono unahitaji umakini wa muda.

Anasema iwapo utachelewa kuunganisha mikono baada ya kuitoa, seli zake zinaweza kufa na kushindwa kufanya kazi zitakapopandikizwa kwenye mwili.

“Katika hili, dawa za kuufanya mwili kukubali mikono hiyo lazima zipatikane kwa sababu mwili una tabia ya kukataa vitu vigeni,” alisema.

Profesa Kahamba alisema upandikizaji wa aina hii ni mkubwa na unahitaji ushirikiano wa kada kadhaa za wataalamu wa afya na vitendea kazi sahihi na vya kisasa.

“Upandikizaji huo ni sawa na sayansi ya kupandikiza mbegu tofauti za miembe, lakini ni mgumu ingawa kwa sayansi ya sasa jambo hilo linawezekana kabisa,” alisema.

Alisema ili Tanzania iweze kufanya upandikizaji kama huu hatuna budi kuweka kipaumbele kwenye sekta ya afya.

Upasuaji wa India
Inaelezwa kuwa upasuaji uliofanyika Kochi uliofanywa na madaktari 20 na kudumu kwa saa 16, unamuwezesha mtu kuisogeza mikono yake baada ya misuli kufanya kazi na kudhibiti mfumo mzima wa fahamu mikononi.

“Hisia zake zinarudi taratibu na baada ya miezi mitatu. Pia atapewa dawa maalumu za kuzuia mwili kuikataa mikono mipya. Dawa hizo zitakuwa zikipunguzwa kidogokidogo baada ya miezi mitatu kumalizika,” alisema ProfesaIyer.

Daktari wa mifumo ya fahamu Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, Harrith Mwinjuma alisema upandikizaji wa aina hiyo umewahi kufanikiwa kwa kutumia vifaa vya umeme akitolea mfano wa Mwanariadha wa Afrika Kusini, Oscar Pistorius ambaye anatembea kwa kutumia miguu ya bandia inayotumia umeme lakini si ya binadamu.

“Hata hivyo, yapo mambo mengi ya kuangalia tunaposema imefanikiwa, hatuangalii tu upandikizaji, bali lazima tuangalie iwapo mikono imefanya kazi. Je, mwili haujaikataa?” alisema Dk Mwinjuma.

Kuhusu umri, Profesa Kahamba alisema wakati wa upandikizaji, madaktari huangalia kigezo cha umri. Kwa mfano, kijana mwenye miaka 30 hawezi kupandikizwa mikono ya mtu mzima mwenye miaka 60 ingawa mzee anaweza kupandikizwa mikono ya kijana.

“Kigezo cha umri ni cha muhimu kwa kuwa seli za mzee huwa zimechoka hivyo kiungo chake kikipandikizwa kwa mtu mwingine hakitakuwa na utendaji mzuri,” alisema.
Historia ya upandikizaji

Kazi za upandikizaji wa mikono zilizofanikiwa katika nchi za Ulaya, China na Australia ni 110 tu, wakati mafanikio ya kwanza yalionekana huko Ufaransa miaka 13 iliyopita.

Oktoba 12, 2012 madaktari wa Hospitali ya Massachusetts walimfanyia upandikizaji wa mikono Joe Kinan (43), ambaye aliungua na kupoteza mikono yake mwaka 2003.

Taasisi ya Tiba ya Sayansi, Mexico, walifanikisha upandikizaji kama huo kwa Gabriel Granados (52), aliyepata ajali ya moto mwaka 2012.

Ronald Thurman wa Indonesia alifanyiwa upandikizaji wa mkono wa kulia katika Hospitali ya Chuo cha Tiba cha Louisville. Upandikizaji huo uliochukua saa 15, ulifanywa na madaktari bingwa 24.
 Na Dk Samuel Shita, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post