Katika hali isiyokuwa ya kawaida afisa mtendaji wa kata ya Kamwanga Sabini Ndaki amechezea kichapo kikali
kutoka kwa mratibu wa TASAF wilaya ya Geita Mkoani Geita Damiani Aloyce kwa
maelezo kuwa amenyima fedha za kumsainia muhtasari
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana katika ofisi za TASAF
Mjini Geita, saa 9:00 alasiri, ambapo mtendaji huyo alikwenda kwa mratibu huyo
ambaye pia ni mlezi wa kata hiyo, ili amsainie muhtasari wa vifaa vya ujenzi wa maabara katika kata ya
Kamwanga ambapo alimwomba Shilingi laki tano ili amsainie.
Akizungumza kwa shida kwenye wodi namba tano katika hospitali
ya wilaya ya Geita Ndaki alisema kuwa alifika kwenye ofisi za Tasaf kwa lengo
la kusainiwa muhtasari uliopitishwa kwenye kikao cha kata kwa ajili ya vifaa vya
ujenzi wa maabara.
“Nimeshambuliwa kwa kipigo na mratibu kwa kosa la kumnyima sh.
Laki tano alizoniomba ili asaini
muhtasari niliompelekea ili nikachukue vifaa vya ujenzi jambo ambalo
nilikataa, kukataa hivyo alinifukuza huku akinisukuma nikadondoka chini, akanyanyua kiti na kunipiga, mkono wangu umepata majeraha na
nina maumivu makali kwenye mwili wangu”alisema Ndaki.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Adamu Sijaona alithibitisha
kumpokea majeruhi huyo na kwamba hali yake inaendelea vizuri .
Kwa upande wake Diwani wa Kamwanga Dionizi Bugali kupitia CHADEMA alikiri
kuwepo kwa tukio hilo la kupigwa mtendaji wake, ambapo alilaani kitendo hicho
na alisema jambo hilo ni la aibu na
ametaka uchunguzi ufanyike haraka ili mhusika achukuliwe hatua kali za
kisheria.
“Jambo hili limenisikitisha kweli kwanza ni kitendo cha aibu
na haya mambo yamekuwa yakijitokeza ya watendaji kuombwa rushwa ili kupitisha
miradi mbalimbali kwa hali hii hatuwezi kufika popote”alisema Bugali.
Waandishi wa habari walimtafuta Kaimu Mkurugenzi wa
halimashauri ya wilaya Deusi Seif ili kutaka kujua kama suala hilo limefika
kwenye ofisi yake, ambapo alisema hajapokea taarifa hiyo na kwamba
atalifuatilia sakata hilo.
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita
Social Plugin