Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia mganga wa
kienyeji Zacharia Ngobeko Dogo(35),mkazi wa kijiji cha Mbulu kata ya Mhongolo
wilayani Kahama kwa kosa la kukutwa na bunduki aina ya SMG yenye namba 8945
iliyotumika katika mauaji ya Mary
Kashindye aliyeuawa kwa kupigwa risasi hivi karibuni wilayani Kahama.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha(Pichani) amesema
mganga huyo wa kienyeji alikamatwa akiwa na silaha hiyo ikiwa na risasi nane
ndani ya magazine iliyokuwa imehifadhiwa nyumbani kwake tarehe 18,2015 saa saba
mchana.
Kamanda Kamugisha amesema mganga huyo na wenzake wawili
wanatuhumiwa kuhusika katika matukio ya mauaji yaliyotokea tarehe 8 mwezi huu
saa tatu usiku kwa kumuua Mary Kashindye kwa kumpiga risasi kutokana na ugomvi
wa kiwanja kati ya marehemu na Jumanne Maige.
Amesema kutokana na ugomvi huo aliwakodi Andrew Buteye
Mtakatifu(38) mkazi wa Tabora na Daudi Luchemela Ngasa(40) mkazi wa Nzega
Tabora kutekeleza mauaji hayo.
Ameongeza kuwa silaha hiyo pia ilitumika katika unyang’anyi
wa kutumia silaha wa tarehe 13 mwezi huu saa mbili usiku wilayani Kahama ambapo
walipora shilingi milioni moja na nusu dukani kwa Manyangu Mboje.
Kamanda Kamugisha ameeleza kuwa katika mahojiano na
watuhumiwa,wamekiri kuhusika katika matukio yote mawili na kuhifadhi silaha kwa
mganga huyo wa kienyeji.
Katika hatua nyingine amesema watuhumiwa wamekiri kutenda
makosa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha katika mkoa wa Mbeya,Mwanza na Tabora.
Na Kadama Malunde-Shinyanga