Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA MKOA WA SHINYANGA AFUNGA KIWANDA CHA UCHENJUAJI DHAHABU CHA BUSHUSHU MJINI SHINYANGA

Eneo la kuhifadhi maji yenye sumu ya kuchenjulia dhahabu katika mradi mmoja wapo uliopo kata ya Ngokolo manispaa ya Shinyanga, ni eneo la makazi ya watu ambalo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga ameufunga rasmi mradi huo na kuagiza mmiliki wake kufikishwa mahakamani kwa kuvunja taratibu za kisheria.

Afisa kutoka ofisi ya madini Mkoa wa Shinyanga akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga( mwenye suti) juu ya mradi mwingine wa kuchenjua dhahabu eneo la Bushushu katika Manispaa ya Shinyanga

Sehemu ya maabara inayotumika katika uchenjuaji wa dhahabu, mmiliki wa mradi huo

 Nyumba hii ndiyo kiwanda chenyewe, awali ilijengwa kwa matumizi ya makazi lakini mmiliki alibadili matumizi na kuamua kuanza kuchenjua dhahabu
Serikali Mkoani  Shinyanga imefunga rasmi shughuli za uchenjuaji dhahabu katika eneo la Bushushu kata ya Ngokolo, manispaa ya Shinyanga  baada ya kujengwa katikati ya makazi ya watu hivyo kuleta athari kwa wananchi kutokana na sumu kali inayotumika kwa kazi hiyo.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga amefunga shughuli hizo mapema leo baada ya kutembelea eneo hilo na kujiridhisha kuwa hapastahili kufanya kazi za aina hiyo na amesema amefanya hivyo ili iwe fundisho kwa wengine.

Rufunga amesema uamuzi huo unafuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi wa eneo hilo kuwa kuna viwanda vinavyojihusisha na uchenjuaji wa dhahabu ambapo Halmashauri ya Manispaa ilishawasimamisha wamiliki wake kuendelea na shughuli hizo lakini walikaidi, hivyo aliamua kufanya ziara akiambatana na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Bi Anna Rose Nyamubi pamoja na wataalamu wa manispaa ya Shinyanga.

Akiwahoji wamiliki hao ambao ni Kija Makindo wa Nyoda Investment pamoja na Ezekiel Allen William (Mbwambo) kwa nyakati tofauti alipotembelea kwenye viwanda hivyo, walikiri kuwa, awali walinunua viwanja hivyo kwa ajili ya kujenga makazi lakini walibadili matumizi na kufanya viwanda vya kuchenjua dhahabu. 

Aidha, Mkuu wa Mkoa ameagiza Mbwambo kupelekwa mahakamani kwa kosa la kuendesha mradi huo bila leseni ya Ofisi ya Madini Mkoa ambao walimsimamisha tangu mwezi Novemba mwaka jana ili wakamilishe taratibu za kutoa leseni lakini alikaidi amri hiyo na kuendelea kuzalisha.

Ofisi ya Mazingira Manispaa pia imedai iliwashauri wamiliki hao kufuata taratibu zote za tathmini ya athari za mazingira kwa kuwasiliana na Baraza la Mazingira la Taifa yaani (NEMC) ili wapate vyeti lakini wameshindwa kufanya hivyo.

Hata hivyo, mmiliki mmoja Makindo ameomba kupewa muda zaidi ili akamilishe taratibu za kuhamisha vifaa kabla ya kufunga kiwanda chake ambapo amepewa siku 30 ili kukamilisha shughuli hiyo.

Na Magdalena Nkulu,Ofisi ya Mkuu wa MkoaShinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com