Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTOTO AUA BABA YAKE MZAZI KWA KUMPIGA NA KOLEO KICHWANI KISA WIZI HUKO TARIME

Mkazi wa Kitongoji cha Nyamorege kilichopo Mtaa wa Forodhani mji mdogo wa Sirari Wilaya ya Tarime mkoani  Mara, Marwa  Kihiri Mwita,  anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi Kihiri  Mwita kinyama kwa kumpiga na koleo kichwani na ubavuni.
Vilevile inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alijeruhiwa kwa kucharangwa kwa panga na baba yake huyo kabla ya kumjeruhi kwa kumpiga na koleo kichwani na ubavuni baada ya kuzuka ugomvi baina yao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Forodhani  Sirari,   Nyangoko Paulo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Ijumaa ya wiki iliyopita jioni katika  kitongoji hicho.
Paulo alisema kuwa ugomvi huo uliibuka baada ya baba kumtuhumu  mwanaye kuwa  anatabia ya wizi.
Alisema inadaiwa kuwa baba huyo alimweleza mwanaye huyo kuwa aliwahi kufanya wizi kitendo kilichosababisha kutozwa faini ya ng'ombe.
Paulo alisema inadaiwa kuwa baada ya baba kutoa tuhuma hizo, mwanaye alitoroka na kuwa nje ya familia kwa zaidi ya miaka mitano.
Alisema aliporudi nyumbani kwao, baba alikerwa na kuanza kumfukuza kwa panga ili asiingie ndani kwake huku akisisitiza aende  akaishi kwa wahalifu wenzake.
Mwenyekiti alisema baba akirusha panga na kumkata mkononi, mwanawe alichukua koleo na kumpiga nalo kichwani na ubavuni.
Alisema majirani walijitokeza kumuokoa na kuwakimbiza Hospitali ya Wilaya Tarime ambako alikufa kabla ya kuanza kupatiwa matibabu.
Polisi Tarime Rorya  wamethibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kumshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano kisha atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Via>> Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com