Kamanda wa Polisi Mkoani kigoma, Jafari Mohamed.
Wanafunzi sita, mwalimu wao, wamekufa papo hapo na wengine 11
kujeruhiwa kwa kupigwa na radi darasani wakati mvua kubwa zilizoambatana
na kimbunga zikinyesha.
Tukio hilo lilitokea saa 2:30 asubuhi katika Shule ya Msingi
Nyakasanda iliyopo kijiji cha Nyaphenda wilaya ya Kasuru mkoani Kigoma
wakati mwalimu huyo na wanafunzi hao wakiwa darasani.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, John Ndunguru, alisema kuwa tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita wakati mvua
hizo zikinyesha.
Alisema mazishi ya mwalimu huyo na wanafunzi hao, yatafanyika leo
mchana katika kijiji hicho chini ya usimamizi wa kamati ya ulinzi ya
mkoa huo.
Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Jafari Mohamed, amethibitisha kutokea
kwa tukio hilo.
Hata hivyo Mohamed, alisema majina ya waliokufa
yatafahamika leo wakati wa mazishi yao.
Vilevile alisema wanafunzi wengine 10 na mwalimu wao waliojeruhiwa
katika tukio hilo, wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa huo ya Maweni kwa
matibabu.
Wakati huo huo; watu wanaoshukiwa kuwa majambazi, wamemuua kwa
kumpiga kwa kitu chenye ncha kali Katibu wa Chama cha Wamiliki wa
Daladala Mkoa wa Kigoma (Kiboa), Maneno Jackson.
Kamanda huyo alisema kuwa mauaji hayo yalitokea usiku wa kuamkia
jana baada ya majambazi hayo kuvamia nyumbani kwa Jackson eneo la
Nazareti Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Alisema polisi wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha mauaji hayo.