RAIS KIKWETE AONGOZA MAZISHI YA CHIFU WA WAHEHE, MTOTO WA MIAKA 13 ATAWAZWA KUWA CHIFU WAO


Mwanafunzi wa Darasa la Saba, Adam Abdul Sapi (13) ametawazwa kuwa Chifu mpya wa Wahehe, akirithi nafasi ya baba yake, aliyefariki na kuzikwa mkoani Iringa.

Rais  Jakaya Kikwete alishiriki maziko ya Chifu huyo wa Wahehe, Abdul Sapi Mkwawa (66)  yaliyokwenda sanjari na hafla ya kumsimika mtoto huyo kushika wadhifa huo wa kimila.
 
Maziko ya kiongozi  huyo aliyefariki Februari 14, mwaka huu, yalifanyika katika kijiji cha Kalenga, nje kidogo ya mji wa Iringa ndani ya makumbusho yaliyowekwa  fuvu la babu yake,Chifu Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga Mkwawa.
 
Mbali na Rais Kikwete, wengine waliohudhuria maziko hayo ambayo taratibu zake zilitumia takribani saa 2.30 kuanzia saa 7 mchana ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Tanzania Bara, Phillip Mangulla, wakuu wa mikoa ya Iringa na Mbeya na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa.
  
Kabla ya kifo chake kilichosababishwa na maradhi ya sukari na figo, Abdul Sapi Mkwawa aliyekuwa mtoto wa tatu wa Spika wa kwanza mweusi nchini, Adam Sapi Mkwawa, alikuwa akifanyakazi katika kiwanda cha maji Afrika cha Kidamali, Iringa.
 
Amewahi pia kufanyakazi katika Chama cha Wazalishaji Tumbaku Iringa na Shirika la Elimu Supplies.
 
Alizaliwa Mei 4, 1949 katika kijiji cha Kalenga na kupata elimu ya msingi katika shule za Kalenga na Tosamaganga kati ya mwaka 1956 na 1963.
 
Mwaka 1964 hadi 1970 alijiunga na shule ya sekondari Iyunga na Mkwawa, ambako alipata elimu ya kawaida na ya juu ya sekondari kabla ya kujiunga na elimu ya juu ya biashara na utawala 1971 hadi 1973.
  
Mmoja wa ndugu wa marehemu, Hussein Sapi alisema mpaka umauti unamkuta, Abdul Sapi Mkwawa alikuwa mtwa (chifu);  alisimikwa mwaka 1999 baada ya kifo cha baba yake, Adam Sapi Mkwawa aliyefariki Juni 25, 1999.
 
Kabla ya maziko ya Chifu huyo, wazee wa kabila la Wahehe walimsimika Adam ambaye ni mtoto wake wa tano kuwa chifu mpya wa kabila hilo.
 
Hata hivyo, mtoto huyo anayesoma katika shule ya msingi ya Highlands ya mjini Iringa, atalazimika kusubiri kufanya shughuli za kichifu mpaka atakapotimiza umri wa miaka 20.
 
Tangazo lililotolewa mbele ya Rais na ndugu wa karibu wa familia hiyo, Joseph Mungai, ilisema mdogo wa marehemu, Saleh atashikilia wadhifa huo mpaka mtoto huyo atakapofikisha umri huo.
 
Baada ya maziko , Rais Kikwete na msafara wake walizungumza na familia ya marehemu kijijini hapo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post