Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAARIFA KAMILI KUHUSU MWANAJESHI KUUAWA NA POLISI KUJERUHIWA HUKO TANGA

Askari wakiteremka kwenye helikopta ya Polisi katika maeneo ya Machimbo ya Amboni mkoani Tanga jana tayari kwa kudhibiti kikundi cha majambazi wanaoidaiwa kutoka nje ya nchi. Kulia ni eneo la tukio

Hali ya wasiwasi imetanda eneo la Amboni jijini Tanga, baada ya mapambano ya risasi kurindima huku askari mmoja wa  Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ) akipigwa risasi ya tumboni na kukimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga, Bombo lakini baadaye alifariki dunia. 

Mapambano hayo yanadaiwa kudumu zaidi ya saa 48 kuanzia juzi saa 5 asubuhi kwenye maeneo ya maporomoko ya Mikocheni, kijiji cha Amboni umbali wa kilometa 10 kutoka mjini Tanga.



Kamishna wa Operesheni ya Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Paul Chagonja, alithibitisha kujeruhiwa kwa askari polisi watatu, wanajeshi wa JWTZ wawili na mmoja aliyefariki, majeruhi  wamelazwa katika hospitali ya mkoa Bombo.



Hata hivyo, alisema askari wanaendelea na operesheni ya kuwatafuta watu hao wanaodaiwa kujificha kwenye mapango ya Amboni.



Alisema mpaka sasa wameshakamatwa watu watatu wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mishale, pinde na mikuki.



Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta Mganga Mkuu wa Bombo, Asha Mahita, kupitia simu yake ya kiganjaji hakupatikana na wauguzi walikataa kuzungumzia hali za majeruhi kwa madai kuwa sio wasemaji.



Kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Freisar Kashai, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alijibu kupitia simu yake ya kiganjani kuwa bado zoezi la kuwatafuta linaendelea na atatoa maelezo baada ya kutoka katika eneo la tukio.



Hata hivyo, imedaiwa kuwa Kamanda huyo hakuweza kurudi ofisini tangu alipoenda kwenye tukio na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Said Magalula, alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani alisema yupo eneo la tukio na kuahidi kuzungumza baadae.



Magari ya JWTZ yenye askari yalionekana yakielekea eneo la mapigano zikiwemo helikopta za jeshi mbili zilizokuwa zikiranda angani. Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wakazi wa kijiji cha Amboni yalipo mapigano hayo, zinasema ilisikika milio ya bunduki kutoka maeneo hayo.



Wananchi hao walieleza kuwa kabla ya milio ya bunduki waliona vikosi vya jeshi la wananchi JWTZ vikiwa kwenye magari eneo la maporomoko hayo.



Habari za awali kutoka vyanzo vya habari ndani ya jeshi la polisi zilieleza chanzo cha sakata hilo ni askari wa jeshi hilo kuwatilia shaka na kuwatia mbaroni watu wawili waliokuwa wakipita madukani jijini hapa kutafuta mahitaji.



Habari hizo ziliendelea kudai kuwa baada ya kuwatia mbaroni watu hao majira ya saa 5 asubuhi na kuwahoji walibaini kuwa sio raia wema na walipowabana walijieleza kuwapo  wenzao katika maeneo hayo.



Hadi tunaenda mitamboni taarifa zinasema watu watatu wanashikiliwa na polisi  na baada ya kuwahoji wamedai kutumwa na magaidi wa nje.



Aidha taarifa zinaeleza kuwa jeshi la polisi lilikabiliana na kikundi hicho kilichokuwa na silaha za kivita na kulazimika kuomba msaada wa JWTZ.



Hata hivyo, inadaiwa kuwa vikosi vya majeshi bado vipo eneo la tukio wakiwemo viongozi wa jeshi na serikali katika kuhakikisha kuwa hali hiyo inadhibitiwa na kujeresha amani iliyokuwepo.



SHUGHULI ZASIMAMA
Kufuatia tishio hilo, shughuli mbali mbali za wananchi na viwanda zimesimama.



Kiwanda kilichosimamisha uzalishaji ni cha Nelkhant kinachozalisha chokaa.



Aidha, baadhi ya watu wamehama makazi yao kwa hofu ya kupata madhara.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com