Mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Ilola
iliyopo katika wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga Veronica Venance(12)
amefariki dunia kwa kupigwa na mwanafunzi mwenzake wakati wakigombania daftari
darasani kwa ajili ya kuandika dondoo (notes).
Tukio hilo limetokea Februari 24
,mwaka huu saa 7 na nusu mchana katika darasa la tano shule ya msingi Ilola
iliyopo katika kata ya Ilola tarafa ya Itwangi wilaya ya Shinyanga.
Walioshuhudia tukio hilo walisema mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma darasa la tano
alifariki dunia baada ya kupigwa makofi na ngumi sehemu za kichwani na
mwanafunzi mwenzake aitwaye Sophia Mathew(12) ambaye pia ni mwanafunzi wa
darasa la tano katika shule hiyo kutokana na ugomvi uliotokana na kugombania daftari.
Akizungumza na Malunde1 blog, afisa mtendaji wa kata ya Ilola
Mahona Joseph alisema tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi hao wakigombania
daftari ambapo marehemu alikuwa ameng’ang’ania daftari aliloazima kwa
mwanafunzi mwenzake Sophia Mathew kwa ajili ya kuandika dondoo za daftari hilo.
Alisema kitendo cha kung’ang’ania daftari hilo wakati siyo
mali yake kilimkera mwanafunzi mwenzake na kuzua ugomvi kati ya wanafunzi hao
na kubababisha kifo cha mwanafunzi huyo.
Naye mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ilola Magere Jonas
aliiambia malunde1 blog kuwa tukio hilo lilitokea wakati wanafunzi hao wakigombana darasani na kwamba huenda
mwanafunzi huyo aliumia kisogoni baada ya kuanguka wakati wa ugomvi huo.
“Ilikuwa muda wa saa saba mchana wakati wanafunzi wengi
wameenda kula wengine wakiwa bado wako shuleni,walimu walikuwa majumbani lakini
mimi na mwalimu mkuu msaidizi tulikuwa chini ya mti tunapunga upepo,mara akaja
mwanafunzi mmoja akasema kuna wanafunzi wanagombana darasani, ndipo tukaenda na
kumkuta amelala chali darasani” alisimulia mwalimu mkuu.
“Kufuatia hali hiyo tukachukua jukumu la kumpeleka kwenye
zahanati ya Ilola ambapo nesi akatushauri kwenda kituo cha afya cha Bugisi
kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo mwanafunzi huyo lakini tulipofika Bugisi
tukaambiwa tayari ameshafariki dunia,tunahisi pengine aliumia kisogoni”,alieleza
mwalimu Jonas.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Longinus
Tibishubwamu alisema wanamshikilia mtuhumiwa Sophia Mathew anayedaiwa kumpiga
Veronica Venance sehemu za kichwani kwa kutumia mikono yake.
Na Kadama Malunde-Shinyanga
Social Plugin