Kumetokea vurugu za aina yake katika eneo la Ilula mkoani
Iringa kati ya askari polisi na wananchi baada ya mwanamke ambaye hajafahamika
jina kufariki dunia wakati wa oparesheni maalum ya jeshi la polisi kukamata
watu wanaouza na kunywa pombe ikiwemo pombe haramu aina ya gongo mida ya kazi.
Tukio limetokea jana Februari 24,2015 saa sita mchana katika eneo la Ilula wilaya
ya Kilolo mkoa wa Iringa
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa polisi walipofika eneo hilo watu waliokuwa eneo hilo walianza kukimbia kuhofia kukamatwa ndipo polisi mmoja
akamchota mtama mwanamke mmoja aliyekuwa anakimbia,akaanguka na
kufariki dunia hapo hapo.
Kufuatia kifo hicho, wananchi walihamasishana na kuanza
kupambana na askari hao huku wakiwa wamebeba silaha za jadi ikiwemo fimbo na mawe,wakazuia magari
yaendayo mikoani,kuchoma matairi barabarani huku polisi nao wakirusha mabomu ya
machozi kuwatawanya wananchi hao.
Inaelezwa kuwa wananchi hao mbali na kuharibu mali
mbalimbali za polisi ikiwemo kuchoma moto magari matatu ya polisi kituo Ilula na vitu vingine vingi.
Mwakilishi wa Malunde1 blog mkoani Iringa Yonna Mgaya anayefanya kazi Radio Furaha ya Iringa amezungumza na kaimu
kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Pudensiana Protas ambapo kamanda huyo wa
polisi amesema polisi walipata taarifa kuwa kuna uuzaji wa pombe za
kienyeji ikiwemo pombe haramu aina ya gongo na walipofika pale watu wakaanza
kukimbia hovyo.
Kamanda huyo wa polisi amesema wakati wananchi wakikimbia
ovyo ndipo huyo mwanamke akateleza na kuanguka akafariki dunia.
Kamanda Protas mesema polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo na
jina la mwanamke aliyefariki halijafahamika na kwamba watatoa taarifa rasmi juu ya tukio hapo baadaye.
Na Yonna Mgaya-Malunde1 blog Iringa
Social Plugin