Mtoto Christina Kusale (2) amelazwa katika Hospitali ya
Mwananyamala baada ya kufanyiwa ukatili na mama yake mzazi kwa kumkata
sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu makali.
Amesema Ofisa Ustawi wa Jamii wa hospitali hiyo,
Dk Rose Temu kuwa mtoto huyo ambaye anaishi Kinondoni alipelekwa na
majirani baada ya kusikia akipigwa na mama yake.
Temu alisema waliingia ndani na kumkuta mtoto huyo
akilia huku akiwa na majeraha yanayodhaniwa ya kisu na kumsababishia
maumivu hayo.
“Mtoto Christina alifikishwa hospitalini hapa
Februari 22, mwaka huu akiwa na majeraha mbalimbali kwenye mwili wake
ambayo yalikuwa sehemu za usoni, mikononi, kwenye makalio, mapaja na
mgongoni,” alisema Temu.
Alisema amelazwa wodi namba mbili akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Alisema mama wa mtoto huyo anashikiliwa na Polisi
na uongozi wa hospitali unafanya utaratibu ili aende kwa ajili ya
kuchunguzwa kama ana matatizo ya akili.
Social Plugin