Kinyesi kilichokutwa ndani ya nyumba ya mwalimu huyo |
Ama kweli dunia ina mambo, na ukistaajabu ya Mussa kweli utayaona ya
Firauni kwa mwalimu huyu wa Sekondari ya Kibasila Jijini Dar es salaam ambapo katika hali isiyo ya kawaida Mwalimu Gaudensia Missanga
wa shule ya Sekondari Kibasila anayefundisha masomo ya Biolojia na Kemia
amekutwa akiishi na lundo la kinyesi cha binadamu chumbani kwake kwa muda mrefu, katika eneo la Temeke Kisiwani.
Mwalimu huyu anadaiwa kuishi katika chumba ambacho amehifadhi kinyesi hali ambayo inatishia usalama wa afya yake.
Hebu jenga picha, mwalimu wa shule ya Sekondari halafu anaishi ndani na kinyesi! Hivi hii imekaaje?
Tukio hilo la mwalimu huyo kuishi na mrundikano wa uchafu huo liligundulika siku tatu zilizopita eneo la Yombo Kisiwani, Kata ya Sandari wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Jinsi tukio hili lilivyotokea
Mmiliki wa nyumba aliyopanga mwalimu huyo, Ruben Shayo aliliambia gazeti moja hapa nchini kuwa Februari 22 mwaka huu, ulionekana moshi kwenye chumba cha mwalimu huyo, ambapo wapangaji wengine walimjulisha na kwenda kuushuhudia moshi huo ili kuweza kujua chanzo chake.
Alisema baada ya kufika kwenye chumba hicho waliona moshi mwingi ukitokea madirishani na kufanya juhudi za kuingia ndani ili kuuzima moto huo, ambapo walijaribu kumuita mwalimu huyo kwa muda mrefu pasipo majibu, lakini mwalimu huyo hakutoka hadi pale walipomwambia kuwa watakwenda polisi.
Baada ya kuitikia, ilibidi kumuita mwenyekiti wa mtaa ili waweze kuingia ndani kwake kuangalia hali ilivyo kwenye chumba chake.
‘’Tuliona funza wakitoka chini ya mlango wake na harufu mbaya ikitoka na mwenzetu hatujawahi kumuona akioga wala akiingia chooni ndiyo tukabaini hali hii,’’alisema Shayo.
"tulipoingia ndani tukakutana na nguo zikiwa zimezagaa na kuonekana kuwa alikuwa akichoma nguo zake”alisema.
Mbali na hayo pia waliona vyombo mbalimbalia ambavyo vilikuwa vimehifadhiwa kinyesi na mkojo, huku kukiwa na funza na mende wakiwa wamezagaa hadi kitandani.
Pamoja na hayo alivitaja baadhi ya vyombo ambavyo alikuwa amehifadhia kinyesi hicho ni ndoo, sufuria, chupa na mabeseni na harufu kali ya kinyesi ikitapakaa ndani.
Kwa upande wake mwalimu Gaudensia anayetuhumiwa kuishi na kinyesi kinachodhaniwa kuwa ni cha binadamu hakuweza kupatikana kujibu tuhuma hizo na alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa inaita bila majibu.
Tukio hilo limeonekana la kustahajabisha kwa waliowengi kutokana na kitendo cha mwalimu huyo kuishi na uchafu huo ndani ya nyumba yake.
Social Plugin