Kivuko cha Mv Dar es Salaam, kinachotarajiwa kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo, jana kilifanyiwa majaribio ya safari ambapo kilitumia saa tatu, huku ikielezwa kwamba kitakapoanza kutoa huduma kitatumia saa mbili kwa safari moja.
Akizungumza
katika ziara ya ukaguzi wa Kivuko hicho, Waziri wa Ujenzi, Dk. John
Magufuli, alisema wamekifanyia majaribio ikiwa ni sehemu ya maandalizi
ya mwisho.
Baada
ya majaribio hayo kwa mujibu wa Dk Magufuli, wanatarajia ndani ya siku
15 watakuwa wamekamilisha taratibu zote, ambapo kitazinduliwa na Rais
Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuanza huduma.
Alisema
kivuko hicho kilichotengenezwa na kampuni ya Johs Gram Hansen ya
Denmark, kitakuwa na vituo saba hadi kufika Bagamoyo na kinatarajiwa
kupunguza msongamano mkubwa na adha ya usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa
Dar es Salaam na Pwani.
Vituo hivyo kwa mujibu wa taarifa za Wizara hiyo ni Magogoni, Kawe, Jangwani Beach, Rungwe Oceanic, Mbweni, Kaole na Mbegani.
Aidha
Dk Magufuli alisema watahakikisha wanaendelea kuwapa kazi Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kamandi ya Maji, kutokana na
utendaji wao mzuri hasa katika ukarabati wa vivuko na ujenzi wa gati.
"Nawahakikishieni
kwamba tutaendelea kuwapa kazi Jeshi kutokana na utendaji wenu, ingawa
najua maneno haya yanaweza yasiwafurahishe Wakala wa Ufundi na
Umene(Temesa), ila ukweli ndiyo huo," alisema.
Aidha
aliwahakikisha wananchi wa kigamboni kwamba usafiri utaendelea
kuimarika, ambapo pia imetengwa Sh bilioni tatu katika bajeti, kwa ajili
ya ununuzi wa kivuko kingine huku ujenzi wa daraja ukiendelea.
"Tutaendelea
kuimarisha usafiri wa majini ili kupunguza msongamano na foleni katika
barabara... Tunawashukuru sana wananchi kwa kuendelea kuvumilia matatizo
madogo madogo ya usafiri, nawaahidi tutaendelea kutoa ushirikiano, ili
kuhakikisha matatizo hayo yanaisha,"alisema.
Dk
Magufuli alisema kivuko hicho kina vifaa vya kisasa, ikiwemo uwezo wa
kuona jiwe au mlima hata wakati wa usiku na kina mwendo wa kasi.
Kuhusu
nauli, Dk Magufuli alisema kitakapoanza kutoa huduma, watapanga nauli
nafuu ambayo kila mwananchi ataimudu, ili atakayetumia kivuko hicho aone
nafuu kuliko kupanda daladala.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Temesa, Marycelina Magesa, alisema kivuko hicho
kimetengenezwa kwa fedha za Serikali kwa asilimia 100 na kimegharimu Sh
bilioni 7.9 na kinauwezo wa kubeba abiria 300.
Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mushi alisema kivuko hicho
kitasaidia kuinua shughuli za wananchi wa mkoa huo na Pwani kwa
kupunguza foleni, ambazo zimekuwa zikipoteza muda mwingi barabarani.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema kivuko hicho
kimekuja muda muafaka hasa katika Mkoa huo, kwa kuwa Bagamoyo ni eneo
la Ukanda wa Kiuchumi na utakuwa mji wa uwekezaji mkubwa kuanzia Julai
mwaka huu.
Aidha
aliomba Wizara hiyo kuboresha miundombinu hasa upande wa Bagamoyo, ili
iwe rahisi kwa wananchi kwa kuwa kwa sasa hali watalazimika kupanda
magari mawili ili kufika kwenye kivuko.
"Naomba
miundombinu iboreshwe na pawe na usafiri wa moja kwa moja hadi mjini
kwa sababu kwa sasa mtu akitoka mjini, analazimika kushuka Zinga ndiyo
aje hapa Mbegani kupanda kivuko ila ukiwepo usafiri wa moja kwa moja
utasaidia sana," alisema.
Social Plugin