Wanasiasa
wamenyooshewa vidole, wakihusishwa na mauaji ya watu wenye ulemavu wa
ngozi baada ya matukio hayo kuhusishwa na harakati za kuelekea katika
uchaguzi mkuu.
Vyama
vya watu wenye ulemavu pamoja na baadhi ya wadau kutoka vyama vya
siasa, vimetaka Serikali kutopuuzia dhana hiyo ya kuhusisha harakati za
kisiasa na mauaji hayo.
Aidha,
Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania, kimesema kiko katika maandalizi
ya kufanya maandamano ya amani hadi Ikulu kwa ajili ya kumwona Rais
Jakaya Kikwete wapange mikakati ya kutokomeza mauaji hayo ya ukatili .
Akizungumza
katika mkutano ulioandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Walemavu na
Vyama vya Siasa nchini, mwanachama kutoka Chama cha Wananchi (CUF),
Abdallah alisema katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi, alisema albino
wanaishi kwa wasiwasi kutokana na uwezekano wa mauaji hayo kuanza
kuibuka tena kwa kasi.
“Mimi
mwenyewe nina tatizo la ngozi (albino), hivi sasa tuko kwenye kipindi
cha uchaguzi, na tetesi ni kwamba wengi wanauawa kwa imani potofu za
baadhi ya watu kutaka madaraka, tusaidieni jamani ukweli ni kwamba
tunaishi kwa hofu,” alisema.
Alisema
ni vyema Serikali ikaacha kupuuzia tetesi hizo za kuwahusisha baadhi ya
watu wanaotaka madaraka na kuagiza watu wenye ulemavu wauawe kwa imani
za kishirikina.
Alitaka hatua madhubuti zichukuliwe kuokoa maisha ya Watanzania hao.
“Jamani
tujue kuwa hii ni damu inayomwagika ni ya ndugu zetu, kama hatua
zisipochukuliwa inaweza kuwa laana kwa vizazi vyetu. Tukijipanga
Tanzania tunaweza kuwa salama,” alisisitiza.
Mwenyekiti
wa Chama cha Wakulima (AFP), Said Soud alisema jamii inatakiwa
kutambua kuwa ni dhambi watu kufikiria kuwa wanaweza kupata utajiri na
madaraka kupitia mauaji au viungo vya watu wenye ulemavu.
“Hili
naomba likemewe kwa nguvu zote, hii ni dhambi kubwa, sisi wanasiasa
tutumie majukwaa kukemea dhambi hii, lakini pia Serikali nayo itekeleze
kwa vitendo sheria zilizopo na kuwaadhibu vikali wale wote wanaohusika
na dhambi hii,” alisema.
Mwenyekiti
wa Chama cha Walemavu wa Ngozi Tanzania, Ernest Kimaya kwa upande wake
alisema, kwa sasa tatizo hilo linazidi kuwa sugu.
Alisema
tangu mauaji hayo yaanze mwaka 2006, hadi juzi alipouawa Yohana Bahati,
maalbino 76 wameuawa kikatili na watu wasiojulikana.
Ushirikina
Hivi
karibuni, katika semina iliyoandaliwa na Jumuiya ya Serikali za Mitaa
Tanzania (ALAT), baadhi ya washiriki walitaja uchaguzi mkuu kuchochea
ongezeko la mauaji ya wenye ulemavu kutokana na wagombea kutumia mbinu
chafu na dhaifu.
Katika
semina hiyo iliyofadhiliwa na Serikali ya Sweden kupitia Shirika lake
la Kimataifa la Maendeleo na Misaada (Sida), ilielezwa na baadhi ya
wachangiaji kwamba, ongezeko la mauaji ya albino katika kipindi cha
uchaguzi, linatokana na imani potofu miongoni mwa wanasiasa uchwara.
Miongoni
mwa wachangiaji katika semina hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam,
Diwani wa Kata ya Sunya, wilayani Kiteto, Manyara, Mussa Brighton (CCM)
aliyeomba serikali kutafuta mbinu za kudumu za kukabili wanasiasa wa
aina hiyo.
Juzi,
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mkurugenzi Mkazi wa
Shirika la Maendeleo la Umoja huo (UNDP), Alvaro Rodriguez katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, pia aligusia kuwapo taarifa
zinazohusisha wanasiasa na mauaji hayo.
Alisema
mashambulio dhidi ya watu wenye albinism, yanaelezwa kuwa
yanasababishwa na imani za kishirikina na kwamba kutoka mwaka 2000 hadi
sasa, watu 74 wenye ulemavu huo wameuawa.
Maandamano
“Kutokana
na tatizo hili kuzidi kuwa sugu chama chetu kimeanza maandalizi ya
maandamano ya amani na kupeleka kilio chetu kwa Rais ili tuweze
kushauriana utaratibu wa kupata suluhu ya kudumu ya tatizo hili,” alisema Kimaya.
Alisema
katika maandamano hayo watayafanya Machi 2, mwaka huu na kwamba, pamoja
na kupeleka kilio hicho kwa Rais, pia watafanya sala maalumu kwa ajili
ya wote waliopoteza maisha yao kwa kuuawa kikatili.
Social Plugin