Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe (picha kutoka maktaba yetu) |
Imeelezwa kuwa watanzania wengi wanapata magonjwa
yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari,presha,saratani na moyo kutokana na kutozingatia ulaji wa vyakula pamoja
kuendekeza uvutaji wa sigara na kunywa pombe kupita kiasi hali
ambayo imefanya idadi ya wagonjwa kuongezeka kila siku na kufikia asilimia 67.
Hayo yamesemwa juzi na
Dkt Digna Narciss ambaye ni bingwa wa magonjwa yasiyoambukizwa
kutoka katika hospitali ya Amana ya jijini Dar es salaam wakati wa
zoezi la upimaji magonjwa yasiyoambukizwa kwa wakazi wa Shinyanga
lililofanyika katika hospitali ya mkoa huo.
Dkt Narciss alisema magonjwa kama kansa,presha,kisukari na moyo yanasababishwa na tabia ya kutozingatia ulaji wa vyakula vya mboga za majani,uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupita kiasi pamoja na uzito uliokithiri.
Alisema kwa mujibu wa
Shirika la afya Duniani( WHO) utafiti unaonesha kuwa mwaka 2011 watu milioni
300 duniani waligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari na kufikia mwaka
2030 kuna uwezekano wa kufikia watu milioni 520.
Aliongeza mwaka 2011
watu waliobainika kuwa ugonjwa wa presha duniani ni milioni 600 kwa mwaka 2011 na maksio ya
kufikia mwaka 2025 ni watu bilioni moja na nusu.
Naye mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba mwaka 2014 asilimia 12 wa wakazi wa Shinyanga walibainika kuwa na magonjwa yasiyoambukizwa ikilinganishwa na mwaka 2013 ambapo ilikuwa ni asilimia 5.
Dkt Kapologwe
alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuwa na utaratibu wa kupanga lishe, kupunguza unywaji
wa pombe,kutotumia zaidi vyombo vya usafiri na kufanya mazoezi.
Katika hatua nyingine aliwataka wananchi kujitokeza kupeleka watoto wao katika vituo vya afya kwani idadi ya watoto imekuwa ni ndogo kutokana na imani iliyojengeka kuwa watoto wadogo hawana magonjwa hayo lakini wapo baadhi ya watoto wenye kupatwa, ni vyema nao wakapimwa.
Na Kadama Malunde-Shinyanga