Takribani miaka 15 imepita tangu ilipotokea ajali katika kijiji cha Idweli wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, iliyosababisha vifo vya watu walioungua wakichota petroli kwenye gari lililopinduka.
Hata
hivyo, tukio la namna hiyo limejirudia tena kijijini hapo na safari hii
watu wawili, wamekufa na wengine 18 kujeruhiwa wakati wakichota mafuta
kwenye gari lililopinduka.
Lori hilo lilikuwa likisafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda Malawi. Lilipinduka kijijini hapo juzi.
Vifo
hivyo viwili vya wakazi wa kijiji hicho, Maria Pajela (18) na Wiliam
Pascal (38), vimetonesha makovu ya huzuni ya ndugu na jamaa wapatao 40
waliopoteza maisha na kulazimu miili yao kuzikwa kaburi moja, kutokana
na kuharibika zaidi na kushindwa kutambuliwa.
Akitoa
taarifa juu ya ajali ya juzi saa 3 usiku, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Mbeya, Ahmed Msangi alisema waliofariki na waliojeruhiwa, walikuwa
katika harakati za kuiba mafuta kutoka katika gari aina ya Scania lenye
namba za usajili T 891 AQZ likiwa na tela lenye namba T 821 ARF.
Alisema gari hilo mali ya Ailis Sanga, lilipakia petroli yenye ujazo wa lita 41,000, likitoka Dar es Salaam kwenda Malawi.
Lilikuwa likiendeshwa na Zawadi Nyato (46) mkazi wa Sae jijini Mbeya akiwa na utingo wake, Frank Yohana (24) mkazi wa Mbozi.
Baada
ya kufika kijijini hapo, liliacha njia na kupinduka. Dereva na utingo
waliokolewa na kupelekwa kituo cha Polisi Kiwira kupata fomu namba tatu
ya kwa ajili ya matibabu.
Kamanda
alisema baadhi ya wakazi, walivamia lori hilo na kutoboa tangi la
mafuta, hali iliyosababisha mafuta kuanza kumwagika na kusambaa maeneo
mbalimbali ikiwemo kwenye makazi ya watu.
Kwa
mujibu wa kamanda, watu hao hawakujali hatari iliyokuwa ikiwakaribia,
badala yake waliendelea kukinga mafuta kwa kutumia vyombo vyao zikiwemo
ndoo, madishi, karai na madumu.
“Wakati
wakiendelea na harakati za wizi huo,wakazi hao walijikuta wakiwa katika
moto mkubwa baada ya lori hilo kulipuka na hapo ndipo wawili kati yao
wakapoteza maisha na waliosalia kujeruhiwa vibaya,” alisema Kamanda.
Alitaja
majeruhi katika ajali hiyo, ambapo wanaume ni 13 na wanawake watano ni
Shukuru Kanzale (21), Nuru George (30), Asante Boniface (38), Joseph
Jamson (18), Joseph Paschal (30), Siza Kanesa (22),Alex Daud (35),
Oscar Yosia (23), Traiphon Moasi (37) na Samson Mbwila (29).
Majeruhi
wengine ni Veronica Elia (30), Dora Michael(35), Rabsen Ayub (26),
Wasiwasi Spika (32), Asia Anon (20), Bahati Kyando (23),Christopher
Erasto(32) na Melisa Sanane (50) wote wakazi wa kijiji cha Idweli.
Kati
ya majeruhi hao, 16 wamelazwa katika Hospitali ya Misheni Igogwe na
wawili wamelazwa Hospitali ya Serikali Makandana, Tukuyu na hali zao
zinaendelea vizuri.
Katika
tukio la mwaka 2000 katika kijiji hicho cha Idweli, gari
lililohusika lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Malawi. Lilianguka
kijijini hapo, kutokana na utelezi katika mteremko unaoishia kwenye
kijiji hicho.
Tukio
lingine la watu kuungua moto nchini, kutokana na kutaka kujipatia
mafuta ya bure, lilitokea mwaka jana katika eneo la Mbagala Rangi Tatu,
jijini Dar es Salaam la mwaka 2014.
Watu
wanne walipoteza maisha na wengine 21 kujeruhiwa vibaya baada ya
kwenda kuchota mafuta yaliyokuwa yanamwagika wakiwa na ndoo, vidumu vya
lita tano na vyombo vingine bila kuchukua hadhari.
~Mpekuzihuru
Social Plugin