|
Wakiamuliwa |
Albino wakichapana makonde
|
Afisa wa Ikulu akiwazuia albino wasifanye vurugu
Katika hali isiyokuwa ya kawaida,
watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), wamepigana ngumi na mateke wakigombea
kuingia kumwona Rais Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Machi 5,2015 ya saa nne asubuhi ambapo lilianzia kwenye eneo la mapokezi Ikulu mara baada ya
walemavu hao kukaguliwa na kuwekwa kwenye chumba maalumu cha kupumzikia wageni.
Baada ya muda, ofisa wa Ikulu
alifika kwenye chumba walipokuwa walemavu hao akiwa na karatasi yenye orodha ya
watu 15, ambao ndio waliopaswa kumwona Rais.
Kila ofisa huyo alipokuwa
akisoma jina, mhusika alitoka nje ya chumba hicho tayari kwa kwenda kumwona
Rais. Baada ya ofisa huyo kumaliza kusoma majina hayo, alisema: “Hawa ndio
wanaokwenda kuwawakilisha kwa sababu hamuwezi kuingia kundi lote hili.”
Wale wengine walioachwa hawakukubaliana na hali
hiyo basi vurugu ndio likaanzia hapo!
*******
Mapendekezo
kwa Dk. Jakaya Kikwete,Rais wa Jamuri wa Muungano wa Tanzania katika
Kikao chake na Wawakilishi wa chama cha Albino Tanzania, Ikulu
,Tarehe 5/3/2015 __________ Mh. Rais, Kutokana
na kuendelea kushamiri kwa mauaji, ukataji viungo, utekwaji na ukatili
dhidi ya watu wenye ualbino na familia zao, Chama Cha Albino Tanzania
kina mapendekezo yafuatayo kwako:
- Ushughulikiwaji
wa kesi zinazohusiana na mauaji, ukataji viungo, utekwaji na ukatili wa
aina hiyo kwa watu wenye ualbino upewe kipaumbele, kupitia mkakati
maalum, kwamba:
- Mashauri yote ambayo hayajapelekwa mahakamani uchunguzi na upelelezi ukamilishwe mapema na yapelekwe mahakamani;
- Kesi
zilizoko mahakamani zisikilizwe mapema, kupitia mahakama au utaratibu
maalum na kwa watakaokutwa na makosa hukumu itekelezwe mara moja;
- Kuwepo
mpango maalum wa kufuatilia kesi hizi, hasa kupitia Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, ili kutoa msaada wa kisheria ikiwemo kwa wale
ambao hawajaridhishwa na maamuzi ya mahakama waweze kukata rufaa.
- Ulinzi
shirikishi katika jamii uimarishwe katika ngazi zote, kuanzia ngazi ya
vijiji au mitaa zijengewe uwezo ili ziwe na mipango maalum ya kutoa
ulinzi kwa watu wenye ualbino kwa kushirikiana na jamii kwani pia wao
ndio wanaowatambua wageni na kupitia wao ni rahisi hata kupata ushahidi
katika kesi mbalimbali. Ni rahisi pia kupitia kamati hizi kuzitambua
kaya zilizoko katika mazingira ambayo sio salama na kufanya uraghbishi,
ikiwemo kuzihamishia katika makazi salama.
- Serikali
iwe na mkakati maalum, endelevu na shirikishi wa kuelimisha jamii juu
ya ualbino na haki za binadamu na mpango huu wa elimu kwa jamii uwe na
bajeti maalum ambayo itakuwa vyema kwa kuanzia ijadiliwe katika bunge
lijalo la bajeti;
- Wahanga wa matukio haya wakiwemo watoto wasaidiwe ili kuboresha maisha yao na kuwajengea misingi mizuri ya maisha ya baadae:
- Watoto walio katika kambi wasaidiwe kupata mahitaji yao ya msingi kama vile chakula, afya, malazi na mavazi kupitia serikali;
- Kambi
hizi ziangaliwe kwa namna pana, ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo
kupitia vyuo mbalimbali vijana walioishi kwa muda mrefu kambini ili
waweze kujitegemea na pia kupunguza athari nyingine zinazoweza
kutokea,ikiwemo mimba na udhalilishwaji wa kingono kama ambavyo imekuwa
ikiripotiwa katika taarifa mbalimbali;
- Watu
wazima wanaoishi katika kambi hizi wasaidiwe kuishi maisha ya staha,
ikiwemo kupata ajira japo ndani ya kambi hizo hizo ili waweze kujikimu
na kutoa mchango wao kwa kuwatunza watoto wakati huu ambao hawawezi
kurudi nyumbani;
- Wale
waliopata ulemavu au kujeruhiwa serikali iwasaidie waweze kujimudu.
Kuna ambao maisha yao yamekuwa ya magumu sana kwa mambo mengi hivyo kuwa
mzigo mzito kwa familia zao ambazo nazo nyingi ni masikini;
- Kambi hizi zisichukuliwe kama za kudumu,ila zijengewe mazingira ya kutoa elimu jumuishi, kuanzia elimu ya awali;
- Wahanga
na familia zao wapewe ushauri (counseling) kwani wengi huwa
wanaathirika sana kisaikolojia na hapajawa na mkakati wa kuwafuatilia.
- Kwa
kuwa mauaji yanayoendelea yanatokana na imani za kishirikina, na katika
matukio waganga wa kienyeji wanahusika, Sheria ya Tiba Asili na Tiba
Mbadala pamoja na Sheria ya Uchawi zipitiwe upya, zifanyiwe maboresho
ili kuweza kutofautisha vizuri juu ya aina hizi za tiba au huduma, na
jamii ishirikishwe katika uratibu wa shughuli za waganga wa tiba mbadala
au tiba asili.
- Kiundwe
Kikosi Kazi maalum kufanya uchunguzi wa kina kubaini wanaotuma na
wanaoununua viungo vya watu wenye ualbino ili washughulikiwe na kuondoa
kabisa jambo hili ambalo limekuwa na kadhia kubwa kwa watu wenye
ualbino, familia zao na jamii na Taifa kwa ujumla.
- Itengenezwe
kanzidata (database) kwa watu wenye ualbino kote nchini ambayo itakuwa
na taarifa mbalimbali (demographic information), zikiwemo idadi na
mahali (makazi); jinsi na umri; elimu na ajira na; hali ya saratani ya
ngozi, ili kuisaidia serikali na wadau wengine waweze kupanga na
kutekeleza mikakati mbalimbali ya ulinzi na jinsi ya kuboresha maisha ya
watu wenye ualbino kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa letu.
- Tunapendekeza
kukawepo na Kamati Maalum ya Kitaifa, ambayo ni jumuishi, iwe inakutana
kwa vipindi maalum (mara kwa mara) kila mwaka kujadili, kutoa mrejesho
na kuishauri serikali na wadau wengine. Kamati hii iwe chini ya Ofisi ya
Rais au Makamu wa Rais au Waziri Mkuu ili iwe rahisi kuratibu mambo
yake kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu. Kwa
kuanzia, kamati hiyo pia ifuatilie utekelezaji wa mapendekezo haya kama
ambavyo utaona yafaa, Mh. Rais.
Mh.
Rais tunakushukuru sana kwa kutusikiliza. Mapendekezo haya na mengine
yatakayochangiwa na wadau yatasaidia kukomesha mauaji na kuwafanya watu
wenye ualbino na familia zao kuishi kwa amani kama watu wengine. Utayari
wetu wa kushirikiana nawe na serikali yetu kama ambavyo tumekuwa
tukifanya wakati wote hauhitaji msisitizo. _____________ Ernest N. Kimaya Mwenyekiti wa Chama Cha Albino Tanzania |
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com