Kiongozi wa kanisa la Ufufuo na Uzima askofu Joseph Gwajima amefika
katika kituo kikuu cha polisi cha jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
mahojiano na jeshi hilo kwa madai ya kutoa kauli, matusi na maneno
makali kwa kiongozi wa kanisa katoliki nchini Muadhama Polycarp Kardinal
Pengo.
Kundi la waanmdishi wa habari liliweka kambi katika kituo
kikuu cha polisi cha jijini Dar es Salaam kutokana na wito wa jeshi la
polisi kupitia vyombo vya habari kumtaka kiongozi huyo wa kanisa la
ufufuo na uzima kufika kituoni hapo kwa mahojiano kwa madai ya maneno ya
kashfa na matusi kwa kiongozi wa kanisa katoliki nchini.
Kutokana
na adha ya foleni kubwa ya magari katika jiji la Dar es Salaam ilibidi
kushuka katika gari lake na kutembea kwa miguu akiwa na walinzi wake
kutoka katikati ya jiji hadi kituo kikuu cha polisi.
Mara baada ya kuwasili katika kituo hicho alipokelewa kwa mahojiano
ya awali kutoka kwa vyombo vya habari ambapo askofu Gwajima amesema
maneno aliyoyatoa ni ya kumkemea kiongozi mwenzake wa kiroho kwa madai
ya kukiuka msimamo wa viongozi wengine wa dini wa kuikataa mahakama ya
kadhi.
Akijibu swali kuhusu sababu za kufanya hivyo badala ya kutumia
maneno ya kistaarabu askofu Gwajima amedai kuwa maneno aliyoyatoa ni
maneno ya mungu huku akishangazwa na wito wa polisi kwa kuwa maneno hayo
hakuyatoa kwa jeshi la polisi bali kwa kiongozi mwenzie wa kiroho.
Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii kumezagaa picha za video
zikiambatana na maneno ya kashfa kwenda kwa kiongozi wa kanisa katoliki
nchini Muadhama Polycarp Kardinal Pengo jambo lililofanya jeshi la
polisi kumtaka kufika kituo kikuu cha polisi kwa mahojiano zaidi.
Via>>ITV
Social Plugin