Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajima (pichani) leo ameachiwa kwa dhamana baada ya kutolewa hospitali ya TMJ alikokuwa amelazwa baada ya kupoteza fahamu na kisha kupelekwa kituo cha Polisi Oysterbay kwa ajili ya mahojiano.
Akiongea na waandishi wa Habari kwa kujihami mara baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Wilaya kinondoni na kupewa Dhamana na kituoni hapo huku waamani wake waliojitokeza na kumpokea Askofu wao wakijazana,amesema hawezi kutishika wala kuyumba kutokana na vikwazo anavyowekewa na Serikali juu ya kuwatetea anaodai wakristo nchini ambao wamewekewa katiba anayoiita ni mbovu.
“Mimi nimetoka kwa amani nashukuru sana mungu ameniponya salama,ila nasema sitoacha kusema ukweli juu ya wakristo wenzangu ambao wanakandamizwa na mifumo ya Katiba ambayo inaonekana wazi”Amesema Askofu Gwajima.
Askofu Gwajima amewataka viongozi wenzake kuheshimu tamko la Jukwaa la Kikristo na hata yeye mwenyewe amesema ataliheshimu sana.
“Nawaomba viongozi wa dini wenzangu tuliheshimu Tamko hili la kikristo,na endapo tukiwa tofauti tutakuwa tunakwenda tofauti na tunajivunjia heshima kwa jamii ambapo tulionekana kuwa na msimamo mmoja wakati tukilitoa na mimi mwenyewe nawahakikishia nitalitetea mpaka mwisho”ameongeza Gwajima.
Alipoulizwa na waandishi wa Habari kuhusu Afya yake amesema hawezi kuzungumzia Afya yake akasema mwenye ruhusa ya kumsemea afya yake ni daktari wake, akawataka waandishi kutoendelea kumuuliza huku akiwataka waamini wake kushangilia kwa ushindi walioupata anaodai umetokana na nguvu ya mungu.
Kabla ya kulazwa katika Hospitali ya TMJ, Askofu Gwajima alipelekwa katika Hospitali ya Polisi Kurasini na baadaye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambapo yeye na wafuasi wake waligoma na kutaka atibiwe TMJ ambapo kuna daktari wake maalumu.
Baada ya kujisalimisha kwa mara ya kwanza polisi Machi 27, mwaka huu, Askofu Gwajima anadaiwa kuhojiwa kwa staili ya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).
Inaelezwa alihojiwa na makachero tofauti waliokuwa wakipishana katika chumba cha mahojiano na ambao wanaonekana kubobea katika taaluma hiyo.
Wakati akidhani mahojiano yamemalizika, inadaiwa waliingia maofisa wengine kumhoji maswali tofauti tofauti, mtindo ambao unatumiwa zaidi na wapelelezi wa FBI.
Hatua hiyo, pia inadaiwa kuchangia kuzimia kwake ambapo awali alidhani mahojiano yangekuwa ni kuhusu kumkashifu Kardinali Pengo tu.
NA KAROLI VINSENT-DAR ES SALAAM