Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema kuwazuia wananchi kwenda nyumbani kwake kumshawishi agombee urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ni sawa na kuzuia mafuriko kwa mkono.
Lowassa alitoa kauli hiyo nyumbani kwake mjini
Dodoma jana wakati alipotembelewa na kundi jipya kutoka Mbarali mkoani
Mbeya waliokwenda kumshawishi atangaze nia kugombea urais.
Lowassa ametoa kauli hiyo siku moja baada ya
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kusema kuwa kwa kuandaa
makundi ya kumshawishi, mbunge huyo wa Monduli anajua adhabu yake na
anaweza kupoteza sifa za kuwa mgombea urais kupitia CCM.
“Sasa mmekuja siku mbaya kwa sababu jana kuna watu
wamesema maneno mengi mabaya ambayo kwa malezi yangu mimi mambo ya
chama humalizwa kwenye vikao vya chama na siyo kwenye vyombo vya habari.
Mnazungumza, mnaelewana mnatoka pale,” alisema.
“Na utaratibu huu ulioanzishwa na watu, mimi ni
vigumu kuuzuia, utazuiaje mafuriko kwa mikono? Mafuriko yanakuja halafu
nazuia kwa mikono nitaweza kweli? Hawa watu sina hoja nao, sina cha
kuwaambia,” alisema.
Mambo ya chama
Lowassa ambaye hivi karibuni aliweka bayana kuwa
ameshawishika kuwania nafasi hiyo, alisema, “Lakini mambo ya chama
hayawezi kuwa kwenye ma-TV, magazeti na maredio, mara huyu hivi, mara
huyu vipi. Mkiona chama kinakwenda kwa utaratibu huo, ni hatari sana,
CCM ninayoijua mimi ni ya vikao.”
Alisema hakusudii kujibu hizo hoja (za Nape) bali rafiki yake Hussein Bashe amezielezea vizuri.
“Niseme mawili tu yanayonisikitisha wanasema eti
nawaiteni, nakupeni fedha, mimi hela natoa wapi? Lakini kibaya zaidi
nikiweka maturubai hapa ni kosa, mkiwa na viti hapa ni makosa? Na
wanasema nawapeni chakula mambo ya ajabu sana na yanasemwa na watu
wazima wenye heshima
zao,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Juzi walikuwapo vijana 300 hapa, nitawapikia
chakula nitawaweza? Nyie kwa wingi huu mtaenea hapa? Lakini ni vibaya
unamdhalilisha binadamu mwenzako kuwa maisha yake yote ni kufikiria
tumbo. Hamna cha kufikiri isipokuwa tumbo, kwa hiyo mnakuja hapa kwa
sababu mnataka Lowassa awapeni chakula, ni kudhalilisha watu.”
Alisema watu wanaofika nyumbani kwake wanafanya
hivyo kwa utashi, hiari na gharama zao wenyewe na wengine yeye
hawafahamu kabisa.
Lowassa alisema hajawahi kuwaona, wala kuwatuma kufanya hivyo au
kuwaomba kufika nyumbani kwake watu ambao wanamshawishi kutangaza nia
ya kugombea urais.
Ushauri wa Kikwete
Aliwashauri wengine ambao hawajafika wasubiri chama kiseme nini kifanyike kwa watu wanaotaka kuja kunishawishi.
“Kwa sababu Rais (Jakaya Kikwete), alivyokuwa
Songea kule na mimi nilikuwapo kule akasema mkiona hawa hawatoshi muda
upo bado washawishini wengine waingie, sasa mkifanya hivi ni kosa, ni
kampeni.
Ipi si kampeni sasa? “alihoji Lowassa na kuongeza:
“Nawashauri tusiingize mgogoro kwenye chama
tungoje tupate maelekezo, mimi nina uhakika kuwa tutapata nafasi. Hakika
ipo siku Watanzania watapata uhuru wa kusema juu ya mtu mimi. Watapiga
kura zao kusema naam ama hapana.
Kwa hiyo tungojee siku. Nami nina hakika wako Watanzania wengi wanaonipenda.”
Kwa hiyo tungojee siku. Nami nina hakika wako Watanzania wengi wanaonipenda.”
Lowassa alisema, “Kwa hiyo huyo anayepiga kelele
nyingi sijui tutoke chama, sijui tufanye nini? Angojee wanachama wa CCM
na wananchi waamue. Mimi ni mwanademokrasia, ninaamini kwenye demokrasia
lakini pia kwenye utendaji bora.”
Lowassa, ambaye bado anatumikia kifungo cha mwaka
mmoja kutoka chama chake aliwataka watu hao kujiandikisha kwa wingi na
kupiga kura kwa mtu ambaye wanaamini ataweza kuwaongoza kwa kutoa
maamuzi magumu na makubwa kwa faida ya nchi.
Juzi, Nape alisema kitendo cha makundi ya watu
kwenda kumshawishi Lowassa atangaze nia ya kuwania urais ni kinyume cha
Katiba ya CCM.
Alisema kitendo hicho ni kampeni ya wazi ya urais
anazoendelea nazo kabla ya muda kufika na kuonya kama ataendelea
atapoteza sifa za kugombea nafasi ya urais.
Katika kipindi cha wiki mbili sasa kwenye makazi
yake Monduli mkoani Arusha na Area C mjini Dodoma makundi ya watu
mbalimbali yamekuwa yakifika kumshawishi agombee urais baadaye mwaka
huu.
Na Sharon Sauwa-Mwananchi
Na Sharon Sauwa-Mwananchi
Social Plugin