BAADA YA WATOTO 18,POLISI WAWAOKOA WENGINE 11 WALIOKUWA WAMEFICHWA KWENYE NYUMBA HUKO HAI KILIMANJARO


Umati mkubwa wa wakazi wa maeneo mbalimbali ya mji wa Moshi wakishuhudia moja ya nyumba iliyokuwa imewahifadhi watoto wenye umri kati ya miaka 3 na 14 wakipewa mafunzo.
Gari la Polisi wakiwa tayari kwa chochote ambacho kingejitokeza katika harakati za kuwatoa watoto hao katika nyumba hiyo


SIKU chache baada ya kugundulika nyumba iliyohifadhi watoto 18 katika eneo la Pasua mjini Moshi mapya yameibuka baada ya kuwepo kwa taarifa ya uwepo wa watoto wengine katika nyumba nyingine huko  Kibosho wilaya ya Moshi vijijini.

Hayo yanajitokeza ikiwa tayari jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro ,likiwashikilia watuhumiwa wawili ,Abeid Karata(36) na mkewe Aisha William(40) ambao ni wamiliki wa nyumba hiyo kwa tuhuma za kuwafungia ndani watoto hao pamoja na kumiliki kituo ambacho hakina usajili.


Mwalimu mstaafu wa shule ya Msingi,Kilindini,Abubakari Sekievu mkazi wa Tanga ameshikiliwa na jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kuhusika kuhifadhi watoto 11 wa kike katika kituo na kisha kuwapatia mafunzo yanayodaiwa kuwa ni ya dini ya Kiislamu na Ushonaji.

Watoto hao wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17 walikutwa katika kituo kinachojulikana kwa jina la Umm Sukhail kilichopo eneo la Lyamungo,kata ya Kibosho wilayani Hai wakiwa wamehifadhiwa kama ilivyo kuwa kwa watoto 18 waliokutwa katika nyumba moja eneo la Pasua mjini Moshi.

Mbali na mwalimu huyo Polisi pia inawahoji wasichana hao wanaotajwa kutoka mikoa ya Dodoma,Singida ,Tanga,Tabora Mbeya na Kilimanjaro ili kubaini mambo kadhaa kuhusaiana na utaratibu wa kisheria wa uanzishwaji wa shule hizo .

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro Geofrey Kamwela amethibitisha kukamatwa na kuhojiwa kwa Mwalimu pamoja na wasichana hao na kwamba mahojiano yanaendelea kujua kama kituo hicho kimesajiliwa ama la.

Kuhusu endapo watoto hao walikuwa wakihudhulia masomo katika shule za serikali,Kamwela amesema bado Polisi inaendelea kuchunguza kwa kushirikisha maofisa elimu na waalimu ili kupata taarifa za kina za wanafunzi hao kama walikuwa wanahudhuria masomo yao ya kawaida au la.

Katika hatua nyingine Kamanda Kamwela amesema watoto 18 waliokutwa katika nyumba moja eneo la Pasua tayari baadhi yao wamechukuliwa na wazazi wao na kwamba imebainika baadhi yao walikuwa ni wanafunzi katika shule za msingi za Pasua,Kaloleni,Langasani,Jitegemee na Azimio za mkoani Kilimanjaro.

Kamanda Kamwela amesema yapo mambo ambayo yanaendelea kutoa mashaka juu ya kugundulika kwa vituo hivyo kutokana na uwepo wa mambo kadhaa yanayofanana kama mikoa  walikotolewa watoto waliokutwa katika kituo cha kwanza na hiki cha hivi karibuni.

Mambo mengine yanayo tia shaka Kamwela amesema ni aina ya masomo yaliyokuwa yakitolewa katika vituo hivyo pamoja na vitu mbalimbali vilivyokamatwa katika vituo hivyo ambavyo hata hivyo hakua tayari kuvitaja kutokana na masuala ya upelelezi.
 Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post